Katika hali isiyo ya kawaida, mwanamme mmoja mkazi wa Kijiji cha Kiria, Kata ya Mamba Kusini, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, anadaiwa kuwabaka na kuwaingilia kinyume cha maumbile watoto wake wawili wenye umri wa miaka 10 na 13 na kuwajeruhi vibaya.
Mwandishi alivyofuatilia
Ni saa 7:30 mchana nafika nyumbani kwa mwanamme
huyo anayetajwa na baadhi ya watu hapa Moshi kwamba anawabaka watoto
wake.Nabisha hodi, sipati wa kunijibu, baadaye anatokea jirani na
kuniambia wenyewe hawapo, namweleza kilichonileta na anakuwa tayari
kunisaidia.
Jirani huyo ananipeleka kwa msamaria mwema
anayemtunza mtoto wa miaka 13 aliyefanyiwa ukatili na baba yake mzazi
kwa kubakwa na kulawitiwa kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa nikiwa
njiani anasema “Unapomwangalia mtoto huyo huwezi amini kuwa kitendo hiki
kimetendwa na baba mzazi ambaye bila shaka kabla ya kuwa na watoto
aliomba kwa Mungu na alitamani sana kuwa na watoto naye aitwe baba”
Nafika kwa msamaria huyo katika Kijiji cha Kiria,
Kata ya Mamba Kusini, najitambulisha na kumweleza lengo langu,
ananyanyuka na kuingia ndani kuzungumza na mtoto anarudi na jibu
lililonipa uchungu na kunitoa machozi. Anamtaja mtoto jina na kusema
amesema hataki kuongea na mwanamme, kama unataka mwambie huyo mwanamme
atoke hapo nje. Mwanaume anayezungumziwa ni yule ambaye alinisindikiza
kuja hapo kumwona.
Ilinilazimu nimwambie mtu huyo niliyekuwa naye aondoke ili nipate nilichofuata kijijini hapo.
Baada ya kuondoka, mtoto huyo akiwa na uso wa
majonzi alitoka nje na kunisalimia kisha kukaa na kuanza kunieleza
mateso na ukatili wa kutisha aliofanyiwa na baba yake mzazi.
Mateso kutoka kwa baba
Mtoto huyo anasema hakumbuki siku ambayo baba yake
alianza kumbaka lakini anasema ni siku nyingi; mara baada ya baba yake
kutengana na mama yao, zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Anasema baba yake huyo alianza kufanya unyama huo
kwa mdogo wake ambaye sasa ana miaka kumi na baadaye akaanza kumwingia
na yeye na kwamba alikuwa akifanya kwa zamu huku akiwafunga midomo ili
wasipige kelele.
Anasema mara zote alipowafanyia unyama huo alikuwa
na panga pembeni akiwatishia kuwachinja kama watakataa au kusema kwa
mtu yeyote.
Mtoto huyo anaeleza kuwa baba yao alioa mke
mwingine, lakini bado akawa anawaingilia, ndipo siku moja mwanamke huyo
alipomfumania na kupigana nae sana kabla ya kuamua kuondoka na kuachana
naye.