Maombi ya TANESCO kupandisha bei ya umeme kutoka sh 198 mpaka 332 kwa uniti moja yapokelewa kwa hisia tofauti



Maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ya kupandisha bei ya umeme, yamepokewa kwa hisia tofauti za kuungwa mkono na pia kupingwa.


Waungaji mkono maombi hayo ni pamoja na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy aliyesema kulingana na changamoto zinazolikabili shirika hilo, bei ya umeme iongezwe ila kwa kuzingatia kutoa huduma zinazolingana na gharama wanazotoza.


Hata hivyo Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) linapinga maombi hayo likisema ikiwa ongezeko hilo  litakubaliwa, wenye viwanda watashindwa kumudu gharama hali itakayosababisha baadhi yao kupunguza wafanyakazi ili kumudu gharama za uendeshaji.

Mjumbe wa Bodi ya CTI, Dk Samuel Nyantahe alisema hawakubaliani na gharama hizo kupanda kutokana na mambo ambayo walikubaliana awali ikiwamo kuboresha miundombinu yao kwanza kutotekelezwa.

Tanesco imeomba kupandisha gharama za umeme kutoka Sh 198 mpaka Sh 332 kwa uniti moja, ili kumudu gharama za uendeshaji za shirika hilo.

Kwa upande wake Kessy alisema: "Karibu robo tatu ya watu wanaiba umeme, lakini hapa sijasikia mkilizingumzia hilo, sasa inabidi pia mkabiliane na wizi huu, vinginevyo itakuwa ni kuwabebesha mzigo wananchi wasio wezi wa umeme."

Akiunga mkono hoja ya Kessy, mdau mwingine Manyerere Jackton alisema viwanda vingi vimekuwa vikiiba umeme, huku wawekezaji wa viwanda hivyo wakiwa wanakingiwa kifua na wanasiasa wanapotaka kuchukuliwa hatua.

Hata hivyo, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) liliitaka Tanesco kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 90 kwa awamu tatu na kutekeleza ahadi zake za kutoa huduma bora.

Mkurugenzi wa Utafiti wa NDC, Godwill Wanja alisema shirika hilo linatakiwa kuongeza bei kwa awamu tatu badala ya awamu moja, akisema Januari 2014 liongeze asilimia 67.87, Januari 2015  asilimia 12.74 na 2016 asilimia 9.17.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, alisema ufanisi wa sekta hiyo ni kwa faida ya uchumi wa Tanzania  na endapo mapendekezo hayo yatakubaliwa yatakuwa ni kwa faida ya wananchi, Tanesco na Taifa. 
 
Pia aliitaka Tanesco kutafuta vyanzo vingine vya uzalishaji umeme badala ya kutegemea mafuta na maji pekee.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema shirika hilo linaomba kupandisha gharama za umeme ili kukidhi mahitaji na kutoa huduma bora kwa wateja wake.

Aliongeza kuwa kulingana na gharama za uzalishaji kupanda, hasara imeongezeka kutoka Sh bilioni 43.43 mwaka 2011 hadi Sh bilioni 178.45 mwaka 2012, hivyo ni sahihi ongezeko hilo likubaliwe ili iweze kujiendesha kwa faida.

Tanesco imeomba Mamlaka Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuidhinisha ongezeko hilo pia kurekebisha bei za huduma za umeme kila baada ya robo mwaka ili kufidia mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni, bei ya mafuta na mfumuko wa bei.
 
"Ikiwa ombi hili halitaridhiwa, shirika litashindwa kumudu gharama za uendeshaji na hivyo  kutokidhi mahitaji makubwa ya umeme nchini na kutoa huduma zenye ubora unaokubalika kimataifa," aliongeza.

Alisema ongezeko hilo lina manufaa kwa wateja, kwani Tanesco itanunua vifaa vya kutosha kukidhi ongezeko kubwa la wateja, kuboresha mifumo ya usafirishaji na usambazaji umeme ili kupunguza kukatika kwa umeme.

Alisema bei isipoongezwa, kutakuwa na athari mbaya kwa shirika hilo kwani litashindwa kumudu gharama za kuendesha mitambo inayotumia mafuta ambayo ndiyo inakidhi mahitaji kwa sasa.

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger