KIONGOZI wa upinzani nchini Ukraine, Julia Tymoshenko leo ameanza mgomo wa kula chakula, akiwaunga mkono maelfu ya watu wanaopinga uamuzi wa serikali hiyo kuubatilisha mkataba baina ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.
Tymoshenko aliyekuwa waziri mkuu wa Ukraine, amesema ataendelea kugoma hadi hapo Rais Viktor Yanukovych atakaposaini mkataba huo kuhusu ushirikiano na biashara huru na Umoja wa Ulaya.
Ameongeza kusema kuwa iwapo Yanukovych hatosaini mkataba huo tarehe 29 ya mwezi huu wa Novemba, atolewe katika uongozi wa Ukraine kwa njia ya amani na kikatiba, pamoja na wasaidizi wake wa kisiasa na wala rushwa.
Polisi wakipambana na waandamanaji mjini Kiev.
Uamuzi huo umepitishwa baada ya Yanukovych kufanya mazungumzo ya siri na Rais wa Urusi, Vladmir Putin mjini Moscow. Mazungumzo hayo yalikuwa yanasadikiwa kuelezea vikwazo vikali ambavyo Urusi ingeviweka dhidi ya Ukraine, iwapo ingeusaini mkataba huo na Umoja wa Ulaya.
Mkataba huo unaiweka wapi Ukraine?
Mkataba huo wa ushirikiano ungeiweka Ukraine katika nafasi nzuri ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya hapo baadaye na kuiondoa nchi hiyo kuwa mhimili wa kihistoria wa Urusi.
Hata hivyo, Rais Putin anaiona Ukraine kama mwanachama muhimu mpinzani wa kiuchumi katika umoja unaojulikana kama Umoja wa Forodha wa nchi za Ulaya na Asia, ambao tayari unazijumuisha Kazakhstan na Belarus.
Jana jioni, Rais Yanukovych aliwataka wananchi wake kuwa watulivu na kuutetea uamuzi huo kwamba ulizingatia hatari za kiuchumi ambazo nchi hiyo ingezipata iwapo ingevuja uhusiano wake wa kibiashara na Urusi.
Rais Viktor Yanukovych na Rais Vladmir Putin.
Jana Jumatatu, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatanya zaidi ya waandamanaji 100,000 wanaoupinga uamuzi huo wa serikali waliokusanyika mjini Kiev.
Umati huo wa watu unaelezwa kuwa mkubwa zaidi kutokea tangu mapinduzi ya chungwa na baadae Viktor Yushchenko kutoka muungano unaounga mkono mataifa ya Magharibi, kushinda katika uchaguzi wa urais mwaka 2007. DW