GATTUSO: HAKUNA NAFASI YA MWANAMKE KATIKA SOKA, APONDA BINTI WA BERLUSCONI KUPEWA UONGOZI MILAN



KIUNGO wa zamani wa klabu ya AC Milan na timu ya taifa ya Italia, Gennaro Gattuso ameponda nafasi ya mwanamke kuwajibika katika majukumu ya kiuongozi katika soka akionyesha wazi kupinga kuteuliwa kwa Barbara Berlusconi kuwa kiongozi wa Milan.

Barbara, ambaye ni binti wa rais wa Milan, waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi, atafanya kazi sambamba na Adriano Galliani kwa muda wa miaka miwili kitendo ambacho kinaweza kusababisha mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Ariedo Braida kujiuzulu.

Gattuso haamini kwamba uamuzi huo ni sahihi kwa klabu hiyo na amezidi kuiponda Milan kwa kumpa mwanamke majukumu makubwa ndani ya timu yenye nguvu Italia

"Samahani, lakini siamini kama mwanamke ana nguvu katika utawala wa soka," alisema Gattuso alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio. "Hivyo ndivyo ninavyoona. Nafikiri ilitakiwa heshima zaidi kwa mtu kama Galliani."

Kutokana na uteuzi huo wa Barbara, wiki iliyopita Galliani aliandika barua ya kujiuzulu kwa kile kilichoelezwa kwamba binti huyo atakuwa na nguvu zaidi ya uamuzi kuliko yeye kitu alichodhani ni dharau kwake. Hata hivyo, rais Berlusconi alimwomba Galliani kutengua uamuzi huo.

Katika kuweka mambo sawa, Galliani amepewa jukumu la kusimamia miradi yote ya michezo wakati Barbara atashughulikia mambo ya masoko na mengine ya kijamii.

Gattuso mwenye umri wa miaka 35, kwa sasa hana kazi baada ya kutimuliwa kuinoa klabu ya daraja la pili ya Palermo baada ya kutofanya vizuri ndani ya mwezi mmoja. Gattuso pia amewahi kuinoa klabu ya Sion ya Uswisi lakini nako alitimuliwa Mei mwaka huu.

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger