JESHI la Polisi wilayani Kasulu mkoani
Kigoma, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kumnusuru Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa
asifanyiwe fujo. Habari za uhakika kutoka Kasulu zinasema, Dk. Slaa
alijikuta katika wakati mgumu baada ya kundi la vijana wanaokadiriwa
kuwa kumi wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kuzua fujo.
Fujo hizo zilitokea kwenye uwanja wa Kiganamo, wakati ambao Dk. Slaa akiwa amebakiza dakika 15 kumaliza kuhutubia mkutano wake.
Baada ya kukatishwa mara kwa mara, Dk.
Slaa alishindwa kuendelea na kujikuta kwenye wakati mgumu, huku walinzi
wake wakihaha asishambuliwe.
Akizungumza na RAI jana, Msemaji wa
Chadema, Tumaini Makene alisema vijana hao walionywa mara kadhaa na
polisi kuacha kufanya fujo, lakini walishindwa kutii amri.
“Kwa muda mrefu vijana hao waliagizwa na
polisi kuacha kufanya fujo, lakini hawakutii…polisi waliona njia pekee
ni kupiga mabomu ya machozi,
“Inasikitisha kwa sababu wale vijana
waliondoka eneo la mkutano kama mita 60, wakaanza kurusha mawe hovyo,
tunawashukuru polisi kwa hatua walizochukua,” alisema Makene.
Alisema baada ya vurugu hizo, Dk. Slaa alishindwa kuendelea na mkutano wake kabla ya muda kumalizika.
“Ni wazi kama siasa hizi zikiendelea
hivi, taifa hili litafika pabaya, wapo wananchi ambao waliamua kufukuza
wale vijana…tunajua hivi sasa kuna kundi la watu wanapandikizwa chuki
dhidi ya CHADEMA,” alisema Makene.
Alisema Dk. Slaa ameapa kuzunguka nchi
nzima kuimarisha chama pamoja na kufungua matawi kama alivyoahidi baada
ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Alisema Dk. Slaa na msafara wake, wanaingia katika Jimbo la Buhigwe ambako atafanya mikutano ya hadhara.
“Kesho (leo), tunatarajia kuendelea na
mikutano yetu katika jimbo la Buhigwe… taifa hili linaongozwa kwa sheria
hatutakubali kuona kikundi kidogo cha watu kinavunja sheria,” alisema
Makene.
Alisema kesho, Dk. Slaa ataingia katika
Jimbo la Kigoma Kaskazini ambalo linaongozwa na aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu wa chama hicho aliyevuliwa nyadhifa zote, Zitto Kabwe.
“Dk. Slaa amesema haogopi mtu, atakwenda
kwenye jimbo la Kigoma Kaskazini bila wasiwasi wowote, licha ya kuwapo
na vitisho vingi vya uvunjifu wa amani,” alisema Makene.
Itakumbukwa wiki iliyopita, baadhi ya
viongozi wa chama hicho mkoani Kigoma walimshauri Dk. Slaa na msafara
wake kuahirisha ziara hiyo kwa sababu za kiusalama.