Barcelona na Real Madrid wamepigwa faini ya zaidi ya£2.5million kila timu baada ya kuvunja sheria ya kusaini mkataba wa muda mrefu wa haki za matangazo ya TV.
Mikataba hiyo baina ya vilabu hivyo na kampuni ya Mediapro imevunja sheria ya nchi hiyo kupitia mamlaka ya ushindani wa kibiashara - inayokataza kuwepo kwa mkataba wa zaidi ya miaka mitatu baina ya vilabu na kampuni ya matangazo ya TV.
Comisión Nacional de la Competencia imefikia uamuzi kwamba vilabu hivyo viwili, pamoja na Sevilla na Racing Santander, vilivunja sheria iliyotungwa mwaka 2010 inayozuia mikataba ya matangazo ya TV kuzidi miaka mitatu.
Real Madrid imepigwa faini ya £3.2m na Barcelona £2.9m wakati Mediapro watalipa faini ya £5.3m. Sevilla imepigwa faini ya £745,000 na Racing Santander ambao kwa sasa wapo ligi daraja la 3 wakiwa na ukata mkubwa wa uchumi watalazimika kulipa £24,800.
Mediapro inawalipa Madrid na Barça kiasi cha £115m kwa mwaka kwa manunuzi ya haki ya mechi zao za nyumbani lakini vilabu vyote viwili vimeambiwa na mamlaka za Spain kwamba ni lazima viache kufanya dili zao binafsi za matangazo ya TV na kujiunga na vilabu vingine katika dili hizo kuanzia mwaka 2016.
Endapo Madrid na Barcelona watajiunga na vilabu vingine katika dili za matangazo ya TV basi mapato yao yatapungua.