Alishauri Bunge kuibadili sheria `aliyoiasisi`
Asema inatumika kama kichaka cha rushwa
Asisitiza ilitungwa kwa wema, sasa inakiukwa
Asema inatumika kama kichaka cha rushwa
Asisitiza ilitungwa kwa wema, sasa inakiukwa
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Sheria hiyo iliyopitishwa miaka ya 2000, ilitungwa na Bunge
lililoongozwa na Spika Pius Msekwa, wakati Sumaye akiwa Waziri Mkuu na
Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
Aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuzindua album ya waimbaji wa
kwaya zilizo chini ya Umoja wa Vijana wa Kipentekoste katika vyuo vikuu
(UPSF) vilivyopo mjini Morogoro jana, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa hotuba yake iliyopatikana kwa njia ya mtandao, Sumaye
alisema kumekuwapo matumizi mabaya ya takrima hasa wakati wa uchaguzi,
akisema inachochea rushwa. “Leo sote tu mashuhuda wa neno takrima
kutumika kama kichaka cha kujifichia wala rushwa,” alisema.
Aliongeza, “sheria zote hutungwa kwa malengo mazuri, lakini katika
matumizi yake likijitokeza tatizo ambalo halikutegemewa, basi sheria
hiyo hufanyiwa marekebisho au kufutwa kabisa.”
Sumaye alisema, “ni vizuri Bunge letu tukufu sasa likaifanyia
sheria hiyo marekebisho kwa kuliondoa kabisa neno takrima au kuipa
tafsiri na ufafanuzi ulio wazi zaidi, ili wala rushwa wasiitumie takrima
kama kichaka cha kujifichia.”
AKEMEA MAUAJI YA OPERESHENI
Sumaye, amekemea mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola, dhidi ya
raia wasiokuwa na hatia ikiwamo kupitia operesheni zinazolenga kudhibiti
uhalifu nchini.
Sumaye alisema, upungufu wa maadili mema ni tatizo kubwa katika
jamii hivyo ipo haja ya kuweka misingi imara ya kuondokana na tatizo
hilo.
“Leo kuna mauaji ya kutisha yanayotokea bila sababu
zinazotosheleza, kama vile watu kujitoa mhanga na kuua watu wengi wasio
na hatia,” alisema.
Alitoa mfano akisema, “hapa kwetu tumeshuhudia watu wakiteketeza
familia nzima kwa sababu tu kakosana na mpenzi wake, vyombo vya serikali
kufanya mauaji wakati wanafanya operesheni mbali mbali jambo ambalo
wanajua ni makosa.”
MISINGI YA HAKI
Sumaye alisema wapo Watanzania wengi wanaoshindwa kupata haki zao
mpaka `kutoa chochote’, wakiwamo madereva barabarani wanaopata shida
kupita bila kuwahonga baadhi ya askari wa usalama barabarani.
“Na haya yapo katika sehemu na sekta nyingi nchini. Ninapozungumza
haya sijawahi kusema hata siku moja kuwa rushwa hii imeanza sasa na huko
nyuma haikuwepo. La hasha! Rushwa imekuwepo hata kabla ya uhuru na
imeendelea kuwapo hadi leo,” alisema.
Aliongeza, “hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikiri
kuwa hata wakati wa utawala wake rushwa ilikuwepo ila walikuwa hawana
utani katika kukabiliana nayo.”
Alisema ipo haja kukubali kuwa rushwa ni tatizo linaloongezeka kwa
kasi, linaumiza uchumi wa nchi, wananchi na kuvunja heshima na hadhi ya
taifa kwa jumuiya za kimataifa.
AOMBA RADHI
Hata hivyo, Sumaye aliomba radhi kwa kauli aliyonukuliwa Novemba
24, mwaka huu mjini Moshi, akisema Tanzania inaongoza kwa rushwa katika
Afrika Mashariki.
“Hapo niliteleza ulimi naomba radhi kama kuna waliokwazwa na hilo.
Nilichotaka kusema ni kuwa “rushwa ni tatizo linaloongoza Tanzania
katika kuathiri maisha ya watu wengi,” alisema.
AWAASA VIJANA
Aliwaasa vijana kujiandalia maisha yatakayowawezesha kuchagia
mabadiliko chanya katika kuwapo utawala bora na kupiga vita maovu,
kuimarisha uchumi.
Aliyataja mabadiliko mengine kuwa ni katika kupiga vita umasikini, kustawisha ulinzi na amani.
Sumaye alisema, “kwa maoni yangu wasomi wetu hamjachukua nafasi
yenu katika nchi na labda hata katika jamii. Kuna mambo mengi makubwa
yanayotokea katika nchi lakini wasomi mnakaa kimya halafu yakisha
haribika tunatafuta wa kuwanyooshea vidole,” alisema.
Aliongeza, “tuna maprofesa waliobobea wa fani mbali mbali,
madaktari wahadhiri na wanachuo wanaoweza kutufanyia uchambuzi na
utafiti ili kuwa na mchango chanya katika jambo lolote. Nafasi hii
haijatumika ipasavyo na wakati mwingine hata nahisi imetumika vibaya.”
Alisema wanataaluma hao hawapaswi kuwaachia wanasiasa kila kitu
pasipo kukosoa na kuonya, badala yake kuwa mithili ya watazamaji na
baadaye walalamikaji.
AIPONGEZA UPSF
Alisema UPSF ina umuhimu kwa jamii kwa sababu, pamoja na mambo
mengine, inawajenga vijana kiroho ili wawe watu wenye hofu ya Mungu.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi wenye imani wa makanisa ya
Pentekoste Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Vicent Komba, alisema umoja huo
haufungamani na upande wala taasisi ya dini yoyote bali upo kwa ajili
ya kubadilisha watu kwa njia ya maombi na elimu kuweza kumrudia Mungu.
Alitaja baadhi ya mambo ambayo umoja huo umekuwa ukipambana nayo
kuwa ni kuwabadilisha watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya, pombe,
ukimwi na masuala ya kifisadi ambayo yamekuwa ni tatizo kubwa hapa
nchini na kusababisha madhara kwa kundi kubwa la vijana.
Alisema kuwa hali hiyo pia imekuwa ikisababisha taifa kukosa
viongozi bora na wasio kuwa na maadili katika kuwatendea watu haki hivyo
kupitia umoja huo watahakikisha wanarudisha uhusiano chanya baina ya
viongozi na wananchi ili kuleta amani.
Walimhakikishia Sumaye kuwa watakuwa naye bega kwa bega kwa
kumfanyia maombi ili kila kukicha wale wanaokusudia kumfanyia mabaya
wasifanikiwe na yale anayokusudia kuyafanya katika siku zake za usoni
yafanikiwe baada ya kuona mambo mazuri aliyofanya wakati wa uongozi wake
alipokuwa madarakani.