UKWELI WA MAMBOKUHUSU KASHFA YA MADAWA YA KULEVYA; IDD AZZAN.


 MBUNGE wa Kinondoni (CCM), Idd Mohamed Azzan, kwa muda mrefu amekuwa akichafuliwa katika vyombo vya habari na hasa kwenye mitandao ya kijamii, akitajwa kuwa mmoja wa wafanyabiashara wa madawa ya kulevya lakini sasa amesafishwa.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Mohamed Azzan.
Uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), unamuweka Azzan pazuri, hivyo ni dhahiri kwamba mbunge huyo si mfanyabiashara wa madawa ya kulevya, isipokuwa wabaya wake wamekuwa wakimchafua kwa maneno ya rejareja.
MCT, iliagiza Azzan asafishwe na Gazeti la Raia Mwema, vilevile limlipe fidia kwa sababu ndilo lililochapisha habari yenye kichwa cha kuhoji Azzan ni mbunge au muuza madawa ya kulevya?
Uamuzi huo, ulifikiwa baada ya Kamati ya Maadili ya MCT, kupokea malalamiko kutoka kwa Azzan, kupitia wanasheria wa Taasisi ya Haki Kwanza, chini ya Wakili Kiongozi, Alloyce Komba.
MCT ilisikiliza pande zote mbili, yaani ule wa Azzan na Raia Mwema na kutoa uamuzi kwamba habari husika haikuwa imejitosheleza.
Hukumu hiyo ambayo nakala yake tunayo, inasema: “Gazeti limeshindwa kuthibitisha kuwa liliongea na Azzan kabla ya kuchapa taarifa. Majibu yanayodaiwa na gazeti kuwa ya Azzan, yalitoka katika chanzo tofauti bila kuzungumza naye.”

Katika mapitio ya hukumu hiyo, MCT iligusia vipengele vinne ambavyo vilionesha kwamba habari husika haikuwa imekamilika, hivyo uchapaji wake ulikiuka misingi ya taaluma nzima ya uandishi wa habari.
Katika malalamiko ya Azzan, alilalamikia habari husika katika vipengele vitano ambavyo ni;
Mosi; ilikosa chanzo cha uhakika, sahihi na cha kweli.

Pili; hakupewa fursa ya kuulizwa ili naye ajieleze kwa upande wake.
Tatu; habari husika ilijaa maoni ya mhariri mwenyewe na mwandishi wake.
Nne; habari ilidanganya kuhusu mali alizonazo na jinsi ambavyo alizipata.
Tano; habari husika iliingilia haki yake ya kikatiba ya kuwa na uhusiano na watu wengine.

Pamoja na vipengele hivyo vitano, Azzan aliambatanisha maelezo kwenye hati yake ya malalamiko kwenda MCT, akieleza kwamba habari husika ilikiuka maadili na misingi ya uandishi wa habari ambayo inafafanuliwa kwa kina kwenye Kanuni ya Maadili ya Wanahabari Tanzania hususan katika ukurasa kuanzia wa pili mpaka sita.
Azzan alisema, muongozo kwa wanahabari kama alivyosoma katika kanuni hizo ni kwamba habari lazima iwe ya ukweli, uwazi, usahihi, kuhoji pande zote husika, kutokuwa na ubaguzi wala upendeleo pamoja na kutokashifu.

Kutokana na hukumu hiyo, Azzan alizungumza na mwandishi wetu na kueleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa MCT kwa sababu umekuwa wa haki.
“Hili liwe wazi sasa kwamba sijihusishi na biashara ya madawa ya kulevya, mimi mbali na uongozi nilionao kama mbunge, ni raia mwema kabisa wa nchi hii,” alisema Azzan na kuongeza:

“Binafsi napambana na biashara ya madawa ya kulevya kwa sababu kati ya vijana wanaoathirika, wengi wao wanatokea kwenye jimbo langu la Kinondoni. Nataka kuhakikisha vijana wanakuwa salama dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya.
“Sasa kama mimi mwenyewe napambana na hiyo biashara, inakuwaje nituhumiwe? Najua kuna mtandao wa kunichafua, binafsi sipo tayari ndiyo maana niliona hili ambalo Raia Mwema wamelifanya inabidi nilishughulikie kisheria nisafishwe.”

Azzan aliendelea kusema kuwa kilichoandikwa kwenye habari husika kilimshangaza kwa sababu kilitengenezwa kwa makusudi ili kuthibitisha maoni kwamba yeye ni muuzaji wa madawa ya kulevya.
“Ilihojiwa eti kwa nini naishi Magomeni, yaani wanataka ionekane kwamba mimi naishi Magomeni ili niuze madawa ya kulevya, mbona watu wengi wanakamatwa Kunduchi kwa biashara hiyo? Takwimu zinajionesha kuwa Kunduchi imekithiri kwa madawa ya kulevya.

“Ilielezwa pia kuwa nyumbani kwangu kuna wasanii wengi maarufu huwa wanakuja, hapa shabaha kuu ni kuuaminisha umma kwamba mimi nashirikiana na wasanii kufanya biashara ya madawa ya kulevya. Huku ni kuniingilia na kuvunja haki zangu kikatiba.
“Kwa nini niingiliwe haki zangu, kuwa na uhusiano na watu wengi ni haki yangu ya kimsingi. Kama ninawasiliana vizuri na wasanii maarufu ni mimi, haipaswi kugeuzwa vinginevyo. Kuishi popote ndani ya nchi hii ni haki yangu mradi sivunji katiba,” alisema Azzan.

Akaendelea: “Mambo mengi yaliwekwa kunichafua. Mfano, waliandika habari bila hata kuwasiliana na mimi lakini ndani yake wakaweka maneno ionekane mimi ndiye nimesema, haya ni makosa makubwa. Namna hii waandishi wa habari wenyewe wanadhalilisha taaluma yao.
“Unafanyaje udanganyifu mkubwa kiasi hicho? Unawaandikia Watanzania maneno ya uongo ya kutunga halafu unasema hayo yametakwa na Azzan wakati mimi sijaongea! Hii tabia siyo nzuri.”

Akikazia hilo, Azzan alisema kuwa ataendelea kubaki imara na wote wanaopanga kumchafua watashindwa kwa sababu skendo wanayoitumia ya madawa ya kulevya ni feki, maana hajawahi kujishughulisha na biashara hiyo tangu azaliwe.
“Waendelee kunizushia lakini watashindwa, mimi nipo imara sana, ingekuwa nafanya biashara hiyo pengine ningebabaika lakini sitishiki kwa sababu mimi nipo safi, tena naamini hao wanaotunga mambo ya kunichafua baadhi yao ndiyo wahusika wa chini kwa chini.

“Mimi ni mbunge na ninafanya biashara halali. Nilianza kuhangaika na biashara zangu nikiwa kijana mdogo sana, nidhamu yangu ya kujituma kutafuta na kutumia bila kufuja ndiyo imenifikisha hapa. Hawajui nimehangaika kiasi gani kufanikiwa, naumia sana kuzushiwa.”

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger