SUALA
la kuruhusiwa kwa Watanzania waishio nje ya nchi kupiga kura ya maoni
ya kupitisha Katiba mpya, limezua mjadala bungeni, ambapo wabunge wengi
wameonesha wasiwasi na kutaka utaratibu huo usitishwe, kwa kuwa unaweza
kuzalisha mamluki na kuweka nchi hatarini.
Pia,
Spika Anne Makinda na baadhi ya wabunge wazoefu akiwemo Mbunge wa Wawi,
Hamad Rashid Muhammed (CUF), wamewaasa wabunge kuhakikisha kuwa
wanaweka itikadi zao pembeni ndani ya Bunge hilo na kuungana kwa pamoja
katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba mpya.
Aidha,
bungeni hapo kuligeuka uwanja wa kusutana baada ya wabunge watokao
Zanzibar kurushiana vijembe hasa baada ya kuibuka kwa mjadala wa kupinga
kutumika kwa Sheria ya Uchaguzi Zanzibar na Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura katika uchaguzi wa kura ya maoni.
Akichangia
mjadala huo bungeni hapo, Mbunge wa Same Magharibi, Anne Kilango
alitahadharisha juu ya uwezo wa Serikali kuweza kuwafikia Watanzania
wote wanaoishi nje ya nchi na iwapo takwimu na idadi yao halisi ipo.
“Ikumbukwe
kuwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni wengi na wanaoishi duniani
kote si hapo London pekee, humu kwenye Sheria tumesema tutaunda kamati
za kura za maoni, wasimamizi je huko nako tutaweza kuunda kamati hizi
duniani kote? Uwezo huo tunao kweli? Alihoji.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF)
alitahadharisha juu ya kipengele hicho kinachotoa fursa kwa Watanzania
waishio nje ya nchi kupiga kuwa huenda fursa hiyo inaweza kutumiwa
vibaya.
Aidha,
aliwataka wabunge kutumia busara na kuweka itikadi zao pembeni
wanapojadili masuala yanayohusu mchakato wa Katiba ili kutokutoa fursa
kwa watu wenye nia mbaya kuliangamiza taifa.
Alisema
kumekuwepo na watu ambao hawaitakii mema Tanzania na kwamba huangalia
fursa yoyote ya kutokuelewana na kujipenyeza kwa ajili ya kuliangamiza
taifa kwa maslahi yao.
“Haiwezekani
kwa mazingira yoyote kutunga Sheria ikawa kamilifu anayeliweza hilo ni
Mungu pekee, ila kama kuna makosa ni vyema kuweka uzalendo mbele bila
kuingiza siasa na kuyabainisha ili yaweze kufanyiwa kazi,” alisisitiza.
Alisema
haipendezi kutengeneza matabaka na makundi ndani ya chombo hicho kwa
mambo ambayo yanaweza kurekebishwa na matokeo yake kuonekana kwa
Watanzania wote.
“Kwa
sasa kuna familia za Wazanzibari takribani 118,000 waliopo Tanzania
bara na kila familia ina watoto zaidi ya wanane, Zanzibar pia kuna
familia za Watanzania Bara 15,000 wanaishi huko na watoto watano kila
familia, sasa kwa haya tunayoyafanya hapa jamii itaenda wapi? Alihoji.
Aliwaomba
wabunge hao kuhakikisha mchakato huo hauwagawi Watanzania na kuangamiza
taifa kama ilivyokuwa kwa mataifa ya Libya na Iraq ambayo kwa sasa
baada ya kusambaratika maliasili zake ikiwemo mafuta zinatafunwa na
wajanja. Spika Makinda naye alionesha kushangazwa na hali ya sasa ya
Bunge hilo, ambapo kumekuwa na mabishano na majibizano huku hoja muhimu
zinazohitaji kuboreshwa zikiachwa.
“Kuna
wasomi humu ndani jamani wakiwemo wanasheria, tumieni taaluma zenu
kurekebisha, tatizo la Bunge hili kila kitu kinafanyika kivyama. Kosoeni
na kusema tufanye nini, sasa nyie mkilalamika mlipo humu ndani waliopo
nje nao wafanye nini? Alihoji.
Mbunge
wa Viti Maalum, Tauhida Gallas (CCM), alionesha kushangazwa na kauli za
wabunge wengine za kupinga kutumika kwa daftari hilo la kudumu katika
uchaguzi huo wakati daftari na sheria hizo ndio zilizotumika katika
kupiga kura ya maoni ya kupitisha mfumo wa Serikali ya Umoja (SUK)
visiwani humo.
“Masuala
ya Wazanzibari tuachieni wenyewe sie tunajuana, ni Waarabu wa Pemba,
hili daftari na sheria inayokataliwa vilitumika kupigia kura ya maoni ya
SUK, sasa leo kwenye Katiba iweje ikataliwe, wenzetu hebu tuambieni
kuna nini hapa? Alihoji.
Alisema
hata suala la kulaumiwa kwa masheha halina mashiko, kwa kuwa masheha
hao wamekuwa wakifanyakazi bila kuzingatia uchama hali iliyosababisha
kulalamikiwa vyama vyote.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene,
alisisitiza juu ya umuhimu wa suala hilo la Katiba kujadiliwa bila
kuingiza vyama kwa kuwa kwa hali inayoendelea bungeni humo imeonesha
kutokuwepo kwa dhamira ya kupatikana kwa Katiba ya Watanzania.
Mbunge
wa Mkanyageni, Habib Mohammed Mnyaa, alipinga vikali suala la kuachwa
kwa Sheria hiyo ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba kwa kuwa imekuwa
ikipindisha haki ya watu wegi kushiriki kwenye uchaguzi akiwemo Rais wa
Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein.
“Sheria
hii sijui kwanini bado inafumbiwa macho, kwani kupitia Sheria hii Rais
Shein ndio Rais wa kwanza duniani kutojipigia kura kwa kuwa tu
haimtambui,” alisema Mnyaa.