Watanzania watolewa wasiwasi kuhusu Uanzilishi wa Sarafu Moja ya Afrika Mashariki...!!

Watanzania wamehakikishiwa kuwa pamoja na changamoto kadhaa zitakazotokana na maamuzi ya kuanzishwa kwa sarafu moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), thamani ya fedha na mali zao havitaathirika.

Marais wa nchi wanachama wa EAC, Jakaya Kikwete (Tanzania); Yoweri Museveni (Uganda); Uhuru Kenyatta (Kenya); Paul Kagame (Rwanda) na Pierre Nkurunzinza (Burundi) wiki iliyopita walisaini itifaki ya kutumia sarafu moja kuanzia mwaka 2023.


Utekelezaji wake unaleta mabadiliko kwa nchi wanachama kwa kuacha kutumia sarafu yake na kuanza kutumia sarafu moja ya itakayokubaliwa na Jumuiya.

Matumizi ya sarafu moja yatagusa moja kwa moja maisha ya kila mwananchi kwa maana ya fedha yake na mali zake pamoja na mambo yanayozihusu nchi zenyewe kama mikopo, uwekezaji na mengine.

NIPASHE limezungumza na wataalamu mbalimbali wa uchumi nchini kuhusiana na faida na hasara ya matumizi ya sarafu moja.

DK. SEMBOJA
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, amewaondolea wananchi hofu kwamba matumizi ya sarafu moja itaathiri fedha na mali zao kwa matokeo hasi, akisema hakutakuwa na athari zozote kwa kuwa kuna taratibu za kueleweka za kuanzisha mfumo huo.

“Kwanza huwa ni sawa na utaratibu mwingine uliowahi kufanyika nchini wa kubadilisha fedha wakati wa kuingiza fedha mpya,” alisema.

Dk. Semboja alisema nchi husika hutoa muda wa kutosha wa kuingiza fedha mpya sokoni, wakati zingine zikibadilishwa taratibu hadi zile za zamani zinapokuwa zimeondolewa sokoni.

Aidha, alisema kimsingi hakuna tatizo hata kwa upande wa kuthamanisha fedha na hata mali zingine kwa sababu taratibu zinazotumika sasa hivi za kuthamanisha fedha kama Dola ya Marekani na Shilingi ya Tanzania, ndizo zitakazotumika hata wakati wa kuingiza sarafu mpya ya EAC.

“Ni suala la kuthamanisha tu, kwamba kama nyumba yako au gari lako lina thamani ya kiasi hiki kwa Shilingi ya Kitanzania, itakuwa na thamani ya kiasi kile kwa sarafu ya Afrika Mashariki,” alisema.

Akizungumzia iwapo kuna uwezekano wa kutokea matatizo ya kutumia sarafu moja kama inavyotokea kwa sarafu ya Euro, inayotumika katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EA), ukiacha Uingreza, Dk. Semboja alisema:

Hilo si tatizo la kuogopa sana kwa kuwa kuna sheria na kanuni imara ambazo zitawekwa na endapo tatizo hilo litajitokeza litashughuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo,” alisema.

Alisisitiza umuhimu wa kuwaelimisha wananchi ili waelewe maana ya kuingia kwa sarafu moja na kwamba hatua hiyo kama itafikiwa, itatoa mfano mzuri kwa nchi zingine za Afrika na ulimwengu kwa ujumla, na fedha hiyo itaheshimika.

Dk. Semboja alisema kupatikana kwa sarafu moja kutaondoa kadhia ya bidhaa toka nchi wanachama zinazouzwa katika soko la EAC, kununuliwa kwa fedha tofauti.

Hata hivyo, alisema kuwa na sarafu moja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, si kitu kipya kwani, huko nyuma nchi hizo zilitumia sarafu moja wakati zikitawaliwa na wakoloni wa Kiingreza.

Alisema fedha hiyo ilikuwa na thamani kubwa na iliheshimika sana katika eneo hili la Afrika Mashariki, nchi zingine za Kiafrika na dunia kwa ujumla.

Dk. Semboja alisema kuanzishwa kwa sarafu moja kutaondoa ile hali iliyopo sasa ya utofauti wa thamani wa fedha ya nchi moja, katika nchi zingine wanachama.

BENKI KUU
Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Joseph Dk. Massawe, alisema hakuna mwananchi atakaye athirika isipokuwa kila nchi wanachama zitatakiwa kuchukua hatua za kiuchumi ili kufikia vigezo vya kujiunga na umoja huo wa kifedha.

“Tutakapofikia hatua ya sarafu moja mabadilisho ya sarafu mpya kwa ya zamani yatafuata viwango vya ubadilishanaji wa kila sarafu.

Kwa mfano, kama tutaamua kwamba sarafu mpya ni sawa na dola moja, Mtanzania atabadilisha fedha zake kwa kiwango cha Shilingi 1,600 kwa unit moja ya new currency (fedha mpya),” alisema Massawe na kuongeza:

“Kwa kifupi, hakuna mtu yeyote atakayepata hasara. Atabadilisha tu fedha zake mama tunavyobadilisha kwa dola au sarafu nyingine sasa hivi.”

Alisema kuwa utiaji saini Itifaki ya Umoja wa Kifedha ni hatua muhimu ya kutufikisha kwenye sarafu moja ya Afrika Mashariki.

Massawe alisema Tanzania itanufaika sana kwa kupanua soko la kufanya biashara na pia gharama za kufanya biashara zitapungua sana na kuwa vikwazo vya biashara vitaondolewa na kuwawezesha wananchi kupanua biashara na nchi wanachama wa umoja huo.

“Sarafu moja italeta uwazi zaidi katika bei, urahisi wa kulinganisha bei katika nchi za jumuiya na pia urahisi wa kufanya malipo. Pia itatuwezesha kudhibiti mfumko wa bei,” alisema.

PROFESA LIPUMBA
Mtaalamu bingwa wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kama nchi wanachama zitakubaliana kuanzisha sarafu moja, basi utawekwa utaratibu wa kuhakikisha kwamba fedha au mali za wananchi zinabaki na thamani ya sarafu zao za zamani.

“Kwa mfano, hivi sasa tuseme sarafu yetu tunahitaji kwa kuanzia iwe sawa na Dola moja ya Marekani; yaani shilingi moja ya Afrika Mashariki iwe sawa na Dola moja ya Marekani. Kwa Mtanzania mwenye fedha benki atazibadilisha kwa exchange rate (bei ya kubadili fedha) inayotawala wakati tunaingia kwenye sarafu moja,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Kwa hiyo, kama ikiwa ni sasa, utaenda kubadilisha Shilingi zako 1,600 za Tanzania upate Shilingi moja ya Afrika Mashariki. Mkenya atapeleka Shilingi zake 80 apate Shilingi moja ya Afrika Mashariki.

Mganda atapeleka Shilingi 2,500 apate Shilingi moja ya Afrika Mashariki. Mburundi atapeleka Faranga 1,500 apate Shilingi moja ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, zitabadilishwa kwa exchange rate itakayokuwa inatawala wakati maamuzi ya kuanzisha sarafu moja yameamuliwa.”

Kwa hiyo, kama una akaunti yako benki kule itabadilishwa tu. Kwamba, sasa ukienda unapata sarafu ya Afrika Mashariki. Lakini unapata ya Afrika Mashariki kwa exchange rate ambayo imekubaliwa kwamba ndiyo thamani ya fedha ya Tanzania ukilinganisha na fedha ya Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza:

Au tunaweza kuweka kigezo kikawa fedha ya Kenya kwamba, Mkenya akiwa na Sh. 80 apate Sh. 80. Tanzania ukienda na Sh. 1,600 unapata Sh. 20.

Alisema jambo la msingi katika kuwa na sarafu moja, inahitajika kwanza kuwapo na soko la pamoja, ambalo litawaruhusu wananchi wote wa Afrika Mashariki kuanzisha shughuli zao mbalimbali mahali popote wanapotaka katika nchi mwanachama.

“Mtu akitaka kutafuta kazi Tanzania apate kazi kama ni mwananchi wa Afrika Mashariki. Ukitaka kuanzisha shughuli yako ya kilimo Tanzania uweze kama ni mwananchi wa Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza:

“Sasa hilo lina utata. Kwamba hamna makubaliano na hususani kwa Tanzania. Na hili si la serikali tu ni la wananchi. Kwamba pana wasiwasi mkubwa kwamba, ajira Tanzania, vilevile ardhi isiwe huru kila mwananchi wa Afrika Mashariki kupata ajira Tanzania, kupata ardhi Tanzania kuanzisha shughuli zote za biashara anazotaka.

“Sasa ikiwa hilo halijakamilika, ikiwa utashi wa kisiasa wa kulifanya hilo haupo kwa nchi zote za Afrika Mashariki, itakuwa vigumu sana kuweza kuwa na sarafu ya pamoja.”


Profesa Lipumba alikumbusha kuwa chini ya mfumo wa sarafu moja ule uhuru wa nchi moja moja kuamua tu kuchapa fedha kutatua matatizo yake, sasa hautakuwako.

Kwamba serikali inakuwa na uhuru ikizidiwa mambo yakiwa magumu kuweza kuchapisha noti kulipia gharama zake, lakini kwa kutumia sarafu moja hilo litadhibitiwa kuepusha mfumko wa bei,” alisema.

MHADHIRI UDOM
Mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Michael Baha, anasema kuwa
fedha za watu zitakazo kuwa katika mabenki thamani yake itabakia pale pale.

Hata hivyo, Baha alisema suala la utumiaji wa sarafu moja limewahi mno na lisipoangaliwa kwa muda linaweza kuleta matatizo kwa sababu linawagusa wananchi moja kwa moja.

Mhadhiri huyo alisema fedha ni alama ya taifa na pia hizi nchi zinatofautiana katika masuala ya sera za kifedha na kushauri kwamba kuna ulazima wa kuweka sera ya fedha inayofanana. Aliongeza kuwa bado kuna tofauti ya viashiria vya uchumi kama vile pato la taifa, mfumuko wa bei na suala zima la ajira.

“Kwa mtazamo wangu naona suala hili limewahi nasema limewahi kwa sababu kama hizi nchi za wenzetu kwa mfano Umoja wa Ulaya wao walitumia muda mrefu sana kufikia matumizi ya sarafu moja, sisi wenye tofauti kubwa za viashiria vya uchumi tutapaswa kutumia muda mrefu zaidi,” alisema.

Alisisitiza kuwa bila kuwa na sera moja ya fedha, nchi moja ikiyumba itaziathiri nchi zote wanachama na jumuiya kuyumba.

Hata hivyo, alisema sarafu moja ina faida nyingi, kama vile ongezeko la fursa za kibiashara na kuondoa usumbufu wa watu kubadilisha fedha.

“Tanzania na Kenya tunatofautiana katika masuala ya exchange (viwango vya kubadili fedha) kwa hiyo gharama ambayo mtu alikuwa aipate katika kubadilisha fedha inakuwa haipo,” alisema Baha na kuongeza kuwa itasaidia upatikanaji wa bidhaa kwa haraka na pia bila gharama kubwa.

MSHAURI ESAMI
Mshauri masuala ya fedha, Chuo Kikuu cha Uongozi Mashariki na Kusini mwa Afrika (Esami), Thobias Mwanyika, anasema sarafu moja itakapoanza kutumika thamani ya fedha katika akaunti za wateja na zilizoko mikononi mwao itategemea na sera ya kuzibadili kutoka Shilingi ya Tanzania kuziiingiza katika sarafu mpya.

Aidha, anasema itategemea kama kutakuwapo na kodi katika kuzibadili kutoka Shilingi kwenda katika sarafu mpya. Hata hivyo, anasema kuwa utafiti kuhusiana na suala hili unahitajika.

Kwa mujibu wa Mwanyika, matumizi ya sarafu ya pamoja kwa upande mwingine nchi wanachama zitanufaika kwa kuondokana na usumbufu katika kubadilisha fedha.

“Mfano wafanyabishara wengi wanapata shida ukitaka kwenda kufanya shughuli zako katika nchi hizi wanachama, lazima ubadilishe fedha, lakini tukiwa na sarafu ya pamoja hakuna haja ya usumbufu huu,” alisema Mwanyika.

MCHUMI WA REPOA
Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini (Repoa), Rose Aiko, alisema azma ya kuwa na sarafu moja kwa EAC ni suala la msingi kwa kuwa litarahisisha biashara na upatikanaji wa tofauti za bei kwa bidhaa na huduma mbalimbali.

Alisema kuwa na sarafu moja, kutapunguza gharama za viwango vya kubadilisha fedha na kwamba nchi pia zitasimamia kikamilifu uchumi wake na kudhibiti mfumuko wa bei.

Alisema nchi wananchama pia zitajitahidi kudhibiti nakisi ya bajeti na deni la taifa kwa kuwa ni vigezo muhimu vya kuingia kwenye sarafu moja.

“Itakuwa rahisi kujua tofauti ya bei za bidhaa mbalimbali kati ya nchi na nchi, biashara zitafanyika kwa haraka na gharama za kubadilisha fedha hazitakuwapo,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger