MASTAA ACHENI UTOTO KWANI NYIE NI KIOO CHA JAMII, MAPENZI NI MAISHA!

KWENU,
Mastaa wa fani mbalimbali Bongo. Salamu sana. Poleni na mihangaiko ya hapa na pale. Kuna jambo nimelitafakari kwa muda mrefu sana, limeniumiza. Nadhani huu ni muda sahihi wa kuzungumza nanyi kuhusu hilo. Angalau kwa wachache wenye uelewa mnaweza kunisikiliza, kupokea na kuchukua hatua.
Bado hamjachelewa. Nianze kwa kuwauliza; hivi ni kwa nini waume wengi hawataki kusikia wake zao wakijiingiza kwenye mambo ya sanaa? Ni kwa nini binti akianza sanaa, iwe ya kuigiza, muziki au unenguaji, huonekana malaya, mhuni na asiye na staha?
Kwa nini wanaume wengi mastaa wa fani mbalimbali, wakitaka kuchumbia mahali, wazazi huweka angalizo kwa mabinti zao? Ni kwa nini wanaume wanaowaoa wasanii, huwaachisha wenzi wao shughuli za sanaa baada ya kuwaoa?
Haya maswali yanaweza kutoa mwanga wa kile ninachotaka kukizungumza katika barua hii ambayo naamini imewafikia wote. Jibu ni moja, sanaa inaonekana ni uhuni. Lakini ni kweli ni uhuni? Jibu rahisi sana. Sanaa siyo uhuni ila waliopo kwenye sanaa wanageuza kama genge la wahuni.

Sanaa ni yenu wenyewe, mna jukumu la kuilinda na kuiheshimu kwa sababu maisha yenu yapo hapo. Wasanii na watu maarufu kwa jumla Bongo wanatia kichefuchefu kwenye suala la uhusiano wa mapenzi. Hata kama binti alikuwa na heshima vipi, akianza sanaa tu, tarajia mabadiliko.
Utamsikia kwenye kumbi za burudani kila kukicha, utamsikia akihusishwa na wapenzi tofauti kila kukicha, kisa? Eti amekuwa staa. Huo ni utoto.

Utakuta msanii wa kiume, anaunganisha wasanii wenzake wa kike kwenye uhusiano na anawatumia wote atakavyo. Wengine bila haya, hawataki kuwasaidia chipukizi mpaka wapewe penzi. Ni mdudu gani anawasumbua vichwa vyenu?
Zaidi nawaonea huruma wasichana. Tatizo mnashindwa kuelewa umuhimu wa mapenzi ulivyo. Mnashindwa kufahamu thamani ya kupenda na kupendwa katika maisha. Rafiki zangu, mapenzi ni ukamilifu wa maisha halisi.

Hata kama ukiwa na fedha kiasi gani, kama huna unayempenda kwa dhati na hakuna anayekupenda kwa dhati, unajiharibia furaha na burudani ya maisha yako. Hili ni jambo la kisaikolojia ambalo hamuwezi kuliona kwa macho.
Mtu mwenye uhusiano na wenzi wengi kwa wakati mmoja ana matatizo ya kisaikolojia. Anapoteza furaha ya ndani na uwezo wake wa kufikiri unapunguzwa na usaliti wa nafsi na wasiwasi wa kusababisha maumivu kwa mwingine. Mapenzi ni maisha.

Yupo staa mmoja (wa kike) wa filamu niliwahi kuzungumza naye huko nyuma. Nilikutana naye Mango Garden. Ni usiku sana, alikuwa amelewa. Kwa sababu ya pombe, aliweza kuwa jasiri na kunieleza jambo zito linalomtesa.
Aliniomba jambo hilo liwe siri – ilikuwa hivyo kweli. Alinieleza huku analia, namna alivyokuwa kwenye utumwa wa mapenzi na staa mmoja mkubwa wa filamu Bongo. Alisema, pamoja na kwamba anajua kuwa ana wanawake wengine tena wengine anawajua kabisa, aliendelea kuvumilia kwa sababu alimpenda na aliogopa kuwekwa pembeni kwenye sanaa.

Wapo wengi wa sampuli hii. Hata ninyi mnawajua, listi ni ndefu sana. Mnapoteza muda kwa kushindana na kugombania mapenzi badala ya kubuni vitu vipya vitakavyozidi kuwaweka juu zaidi kwenye sanaa.
Wengine wanajidanganya kwamba wakiingia kwenye skendo za mapenzi na waandishi wakanasa na kuandika, watakuwa juu kisanii. Ni mawazo ya kijinga hayo.

Mastaa wa kike waliochakazwa kwenye mapenzi wanajua mateso wanayopata sasa hivi – nani ataoa mmama mtu mzima aliyekuwa akiripotiwa kubadilisha wanaume kila siku? Nani atakubali kuolewa na mwanaume ambaye kila siku anabadilisha wanawake?
Heshima yenu kwenye jamii iko wapi? Acheni uvivu wa kufikiri. Hebu jifunzeni kwa wenzenu wa Marekani, Nigeria, India na Ghana (kwa mfano). Wanaheshimu mapenzi na mara nyingi uhusiano wao huwa wa wazi.

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger