MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage amesisitiza kuwa uamuzi wote uliofanywa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo ni batili na kwamba hautambui pia uteuzi wa Kocha Zdravko Logarusic wa Croatia.
“Nimeshakwambia kuwa maamuzi yote yalikuwa batili, kwa sasa sitambui lolote kuhusu huyo Kocha (Logarusic). Mpaka sasa kocha ninayemtambua ni Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo,” alisema Rage.
Rage alisisitiza kuwa kikao hicho kilikuwa ni batili kwa sababu kilikuwa na lengo la kufanya mapinduzi, hivyo uamuzi wowote ambao ulifanywa na kikao hicho ni batili.
“Mimi kocha ninayemtambua ni Kibadeni na Julio, huyo mwingine simjui,” alisema Rage jana Jumatatu alipozungumza na gazeti la Mwanaspoti.
Kamati ya Utendaji ya Simba chini ya makamu mwenyekiti Joseph Itang’are ilikutana Jumatatu usiku wiki iliyopita na kumsimamisha Rage aliyekuwa safarini Sudan pamoja na kuliondoa benchi lote la ufundi chini ya Kibadeni na Julio.
Hiyo ina maana kuwa ujio wa kocha mpya wa Simba, Logarusic utategemeana na suluhu ambayo inaweza kupatikana baina ya pande mbili ambazo zinapingana kati ya Rage na Kamati ya Utendaji ya Simba.
Kibadeni alipoulizwa alisema; “Ni kweli Mwenyekiti (Rage) amenipigia simu jana (Jumapili) usiku kuniambia kwamba amenirudisha Simba, sikumkatalia maneno yake siwezi kutoa kauli ya moja kwa moja hadi nitakapoona kuna taarifa rasmi ya klabu.
“Unajua wakati napewa kazi Simba nilipewa mkataba pia wakati nasimamishwa kazi hivi juzi pia walinipa barua ambayo imesainiwa na watendaji wa timu, sasa katika hili nalo natakiwa kupewa taarifa kwa njia hiyo,kuna muda inabidi utoe nafasi kwa watu wachache ili wafanye uamuzi wanaouona una manufaa kwao, wao wanadhani mtu mwingine ataipa Simba ubingwa, basi waendelee naye ili watimize azma zao,” alisema Kibadeni.
Akizungumza na Mwanaspoti mwishoni mwa wiki, Kocha Logarusic alikuwa anajiandaa kutua Dar es Salaam Desemba Mosi kuanza kazi ya kukinoa kikosi cha Msimbazi.