MSANII wa muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuandika juu ya uzushi wa kifo cha msanii mkongwe, Said Ngamba ‘Mzee Small’ kupitia mtandao wa Instargram.
Shilole ambaye baada ya kugundua kuwa hakuwa sahihi kuandika juu ya kifo hicho kwani haikuwa kweli, alilazimika kukanusha na ndipo akaanza kuporomoshewa ‘mvua’ ya matusi.
Baadhi ya maneno makali yaliyoandikwa mtandaoni humo kumtukana Shilole, ambayo hayawezi kuandikika gazetini kwa kuzingatia maadili, yalimtaka kujiepusha na tabia ya kudandia na kueneza mambo pasipo kuyafanyia uchunguzi.
“Ni kweli niliandika maneno ya taarifa za kifo cha Mzee Small, japo nilikuwa nikiandika jinsi ambavyo msanii huyo amezushiwa kifo, sasa watu wakadhani mimi ndiye nimeandika kwa kujitungia, najuta sana kuchapisha ujumbe huo,” alisema Shilole.