Kamati ya Bunge yadai TAMISEMI ni sehemu ya mtandao wa ufisadi..


Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), imeilipua Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa madai ya kuwa sehemu ya Mtandao wa Ufisadi serikalini. 
 
Tamisemi inaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia anayesaidiana na manaibu waziri wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim Majaliwa.
Halikadhalika kamati hiyo ya Bunge imesema, zipo dalili za wazi za kuwapo kwa mtandao wa kutisha wa kifisadi unawashirikisha baadhi ya watendaji wa halmashauri nchini, hazina na Tamisemi.

 
Tuhuma hizo zilitolewa Bungeni jana na Mwenyekiti wa Laac,Rajab Mbarouk wakati akiwasilisha taarifa ya hoja za kamati kuhusu hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2012.
 
Alisema bado kuna ubadhirifu,ufisadi na utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa matumizi ya fedha za umma kutokana na Tamisemi kutosimamia ama yenyewe kuhusika moja kwa moja na ufisadi huo.
 
“Mfano mwaka 2011/12, Sh1.6 bilioni zilitumika nje ya bajeti iliyoidhinishwa katika halmashauri 38 na Sh2.6 bilioni zilihamishwa kutoka akaunti moja kwenda nyingine bila kurudishwa,”alisema.
 
Kamati hiyo imebaini kwamba upo mtindo wa Serikali kutuma kwa halmashauri kiasi kikubwa cha fedha kuliko kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na Bunge katika fungu husika wakati wa upitishaji bajeti.
 
Kamati hiyo imetolea mfano wa Sh2 bilioni zilizotumwa Halmashauri ya Jiji la Tanga na Sh500 milioni zilizotumwa katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe ikiwa ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.
 
“Kitendo hiki ambacho kinafanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu wa Hazina,Tamisemi na Halmashauri kinaashiria kuwapo mtandao wa kutisha wa kifisadi baina ya mamlaka hizo,”alisema.
 
Kamati hiyo imeituhumu pia Tamisemi inayoongozwa na Waziri Hawa Ghasia, kuwahamisha haraka watumishi wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kutoka hamashauri moja kwenda nyingine.
 
“Kamati imebaini kwamba Tamisemi imekuwa ikitumia mtindo huu kuwalinda watumishi mafisadi ndani ya halmashauri na kuifanya kamati iamini Tamisemi ni sehemu ya mtandao huu,”imesema.
 
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kwa makusudi,Tamisemi imekuwa ikieneza saratani hiyo ya ufisadi kwenye halmashauri nyingi iwezekanavyo na kuitaka Serikali kuachana na mtindo huo.

Kamati ya Bunge ya Bajeti, imeishauri Serikali kupunguza matumizi na kuongeza ukusanyaji mapato ili miradi ya maendeleo igharamiwe kwa asilimia 35 ya bajeti ya Serikali.
 
Akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo Bungeni jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge alisema kwa utaratibu wa sasa hakuna uwiano sawia kati ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo.
 
Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariad Magharibi(CCM) alisema, mwenendo wa deni la taifa si wa kuridhisha kutokana na kuongezeka kwa mikopo ya masharti ya kibiashara na malimbikizo ya riba.

-Mwananchi

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger