BAADHI
ya wafuasi cha Chadema, jana nusura waanzishe fujo kwenye mdahalo wa
kujadili demokrasia na migogoro ndani ya vyama vya siasa, baada ya mmoja
wa washiriki kutamka kuwa, CCM itaendelea kuongoza nchi endapo vyama
vya upinzani vitaendelea kuwa na migogoro hivyo kuzidi kividhoofisha.
Kauli hiyo, licha ya kutaka kusababisha fujo, iliwafanya baadhi ya wafuasi wa Chadema kutoka nje ya ukumbi.
Rehema
Mwenda wa Chama cha Wananchi (CUF), ndiye aliyepasua ukweli huo
uliowakera baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani, baada ya kusisitiza
migogoro katika vyama haina faida zaidi ya kuvidhoofisha, huku CCM
ikizidi kujipanga na kuonya kuwa, migogoro ikiendekezwa ni sawa na kuipa
CCM fursa ya kuendelea kuongoza nchi.
Katika
mdahalo huo ulifanyika jijini Mwanza ilizuka sintofahamu wakati mtoa
mada ya “Hali ya Siasa - Tulikotoka, Tulipo na Tuendako”, Habibu Change
alipokuwa akiwasilisha mada yake na kudai kuwa ndani ya Chadema kuna
mgogoro, kauli iliyopingwa na Wana-Chadema na wengine kutoka nje kabisa
ya ukumbi wa mjadala.
Akichangia
katika mdahalo huo, Shaban Ironga alisema migogoro ndani ya vyama vya
siasa imekuwa ikidumaza demokrasia ya kweli na mawazo ya kweli kutokana
na maamuzi ya wachache na faida ya wachache.
“Demokrasia
ya kweli hujengwa na wanachama kuanzia ngazi ya chini na kwamba wapo
waliogombana na kupoteza ndugu zao kutokana na vyama hivi lakini leo
wanaonekana sio watu ndani ya vyama kutokana na ubinafsi na maamuzi ya
wachache,” alisema.
Aidha
Ironga aliwataka wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani kuamka na
kuacha kutumika na viongozi kwa ajili ya maslahi yao kwani wamekuwa
wakipoteza nguvu zao huku wanzao wakiendelea kunufaika.
Awali
akitoa mada ya kwanza ya demokrasia na migogoro ndani ya vyama vya
siasa, Jimmy Luhende alisema hakuna siasa ya kupendana kwenye mapambano
na kwamba wakitokea marafiki ujue wanaanza kupotosha jitihada za
mapambano.
Mdahalo
uliokuwa ukijadili migogoro ndani ya vyama vya siasa inakuza demokraia
au la, uliandaliwa na Asasi ya Jitambue Foundation ambapo walilazimika
kuita mabaunsa ili kudhibiti vurugu zilizotaka kujitokeza.
-Habari Leo
-Habari Leo