MADIWANI CCM,CHADEMA WAPIGANA NGUMI KAVUKAVU KISA KUHOJI MATUMIZI YA MILIONI 95/-

 .
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya,Diwani Athuman
Madiwani wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wamejeruhiwa vibaya hadi kulazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa kile kinachodaiwa kupigwa na wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika eneo la ukumbi wa halmashauri wa Mkapa wakati kikao.
Diwani wa Kata ya Mwakibete ambaye pia ni Katibu wa Mwenezi Chadema wilaya ya Mbeya Mjini, Lucas Mwampiki, jana aliwaeleza wandishi wa habari kuwa tukio hilo lilutokea Ijumaa iliyopita katika ukumbi wa Mkapa ambao unamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Mwampiki aliwataja madiwani waliojeruhiwa na kulazwa kuwa ni wa Kata ya Sinde, Fanuel Kyanula na wa Kata ya Ilemi, Furaha Mwandalima.

Mwampiki alisema kabla ya kutokea kwa vurugu hizo, madiwani wa vyama vya upinzani walikuwa wakihoji uhalali wa ziara ya baadhi ya maofisa wa Halmashauri ya Jiji wakiongozwa na Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, kwenda China kwa kutumia fedha za halmashauri bila kufuata utaratibu.

Alisema katika ziara hiyo, Meya Kapunga aiongozana na maofisa watano ambao ni Mkurugenzi wa Jiji, Mchumi, Afisa Mipango na diwani mmoja wa CCM ambayo iliigharimu halmashauri hiyo zaidi ya Sh. milioni 95 ambazo hazikuwa kwenye bajeti wala kuidhinishwa na kikao chochote.

Alisema madiwani wa Chadema na NCCR-Mageuzi walifuata taratibu zote za kuhoji suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuorodhesha majina yao na kusaini ili mkutano wa madiwani uitishwe na hoja hiyo ijadiliwe.

Kwa mujibu wa Mwampiki, kikao cha Madiwani kilichoketi Ijumaa waliamini kuwa ajenda hiyo itaingizwa, lakini wakashangaa kuona haimo kwenye orodha ya ajenda zilizopaswa kujadiliwa.

Alisema madiwani wa upinzani walipohoji juu ya kuondolewa kwa ajenda hiyo, Meya Kapungu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alikuja juu na kuamuru mlango ufungwe ili madiwani wapigane.

“Tulishangaa kusikia Meya akisema kuwa kila siku madiwani wa Chadema tunawafanya wasiishi kwa raha mjini na kutamka kuwa inabidi milango ifungwe ili zipigwe,” alisema Mwampiki.

Alisema madiwani wa Chadema kuona hivyo waliamua kutoka haraka nje ya ukumbi wa mkutano, huku wakirushiwa chupa za maji na baadhi ya madiwani wa CCM.

Mwampiki alidai kuwa hata baada ya madiwani wa Chadema kuwa wametoka nje ya ukumbi wa mkutano, madiwani wa CCM waliwafuata na kuanza kuwashambulia kwa kipigo mpaka walipoachanishwa na polisi waliokuwepo eneo hilo.

Alisema katika vurugu hizo, madiwani wawili wa Chadema walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa kwa matibabu na walilazwa.

Asema Diwani wa Ilemi, Mwandaliwa alijeruhiwa sehemu za shingo kiasi cha shingo yake kutogeuka kila upande huku Diwani wa Sinde, Fanuel akiwa amejeruhiwa kwenye shavu kutokana na ngumi walizokuwa wakipigwa.

Akizungumza baada ya kutoka hospitali, Mwandalima alisema alikuwa miongoni mwa madiwani wa mwisho kutoka ukumbini na kuwa alipofika nje ya ukumbi alijikuta akivamiwa na kundi la madiwani wa CCM ambao walianza kumshushia kipigo huku wengine wakimkaba na kumuumiza vibaya maeneo ya shingoni.

Meya wa Kapunga alikanusha kuhusika na ugomvi huo huku akisema kuwa hakuna diwani aliyepigana ndani ya ukumbi wa mkutano.

Alisema anachokumbuka ni kwamba madiwani wa upinzani walikuwa na hoja ya kutaka kujua juu ya ziara ya watumishi wa Halmashauri nchini China, lakini hawakufuata utaratibu na kanuni  walizojiwekea katika kuhoji masuala mbalimbali ya halmashauri.

Alisema baada ya kupitia orodha ya majina ya madiwani waliokuwa wakihoji suala hilo, walibaini kuwa kuna baadhi ya saini za madiwani zimeghushiwa, jambo ambalo alisema ni kinyume cha taratibu za halmashauri na sheria za nchi.

Alisema miongoni mwa saini zilizobainika kughushiwa ni za baaadhi ya madiwani ambao hawapo jijini Mbeya kwa muda mrefu.

Alisema baada ya hoja ya madiwani hao kukataliwa, ndipo walipoinuka kutoka ndani ya ukumbi wa mikutano huku wakiwatolea matusi ya nguoni madiwani wenzao wa CCM.

“Ninachokumbuka ni kwamba wakati madiwani wa Chadema wakitoka nje walikuwa wakitukana matusi ya nguoni inawezekana matusi hayo yaliwauma wenzao wa CCM ambao waliwafuata huko nje, hivyo kama walipigwa nje ya mkutano mimi sina taarifa,” alisema Kapunga.

Akizungumzia ziara ya watumishi wa halmashauri ya akiwamo yeye nchini China, Kapunga alisema ziara hiyo ilitokana na agizo la serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (Tamisemi).

Alisema kabla ya kufanya ziara hiyo alifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kulijulisha Baraza la Mdiwani la Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Ofisi ya Katibu Tawala ya Mkoa wa Mbeya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza, alipinga kiwango cha fedha cha Sh. milioni 95 kinachodaiwa na madiwani wa Chadema kuwa kilitumika kwenye ziara hiyo, badala yake alisema zilitumika Sh. milioni 54.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema yuko nje ya Mkoa wa Mbeya kikazi, hiyo hakuwa na taarifa zozote.

Pamoja na Kamanda Diwani kusema hana taarifa, lakini Mwandalima alisema walipewa fomu za polisi PF 3 kabla ya kupatiwa matibabu hospitali.

CHANZO: NIPASHE

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger