NYOTA wa filamu na mshindi wa zamani wa Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike nchini, Riyama Ally a.k.a Riyama amewataka wasanii wenzake kuacha tabia alizoziita za kijinga kwa kuiga maisha na uigizaji wa wasanii wa ng’ambo.
Riyama ambaye sifa yake kubwa kwenye ‘game’ ni kuvaa uhusika, hasa wa kumwaga machozi, alisema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalum na gazeti hili jijini Dar es Salaam.
“Usanii si kukaa uchi, unajua baadhi ya wasanii wenzetu wanashindwa kufahamu hilo. Kukaa uchi hakumaanishi ndiyo utaonekana mzuri zaidi,” alisema kwa masikitiko Riyama.
Akizidi kushusha ‘maskadi’ Riyama alisema, tatizo kubwa walilonalo wasanii wa Kibongo ni kuiga, mwenyewe anafafanua: “Haijakatazwa kuiga, lakini unatakiwa kujua unaiga nini. Hatuwezi kuchukua tamaduni za watu na kuleta kwetu. Wao wana miiko yao, nasi pia. Kwanini tuige ujinga?”
Alisema, wasanii kuvaa nguo fupi zisizo na heshima, huua soko la filamu bila la wasanii wenyewe kujua kwani watu wenye heshima zao hawawezi kununua na kwenda nazo majumbani mwao.
Kwa muda mrefu sasa, magazeti Pendwa yamekuwa yakiandika habari kuhusu kero za wasanii kuvaa nguo fupi ambazo zinaacha sehemu za miili yao wazi, lakini wenyewe wamekuwa wakiweka pamba masikioni.