LiverpooL hawakamatiki wawafumua Spurs 5 – 0, wazidi kupaa kileleni

liver_97e50.jpg
*Man United wawashinda Villa kwao
*Arsenal bado hawajaguswa kileleni
London Kaskazini pamekuwa na kilio baada ya Tottenham Hotspur kusababishiwa mafuriko na Liverpool waliofika White Hart Lane kwa mchezo wa ligi.
Tofauti na matarajio ya maelfu ya washabiki waliofika wakijua wangeibuka na ushindi, mambo yalikwenda kinyume kabisa.
Liverpool kutokuwa na nahodha wao Steven Gerrard na mshambuliaji mahiri Daniel Surridge kutokana na majeraha kulidhaniwa kungewafaidisha Spurs.
Hata hivyo, vijana hao wa kocha Andre Villas-Boas walioshuka dimbani kwa kujiamini, waliondoka kwa aibu baada ya kunyukwa mabao 5-0.
Luis Suarez aliyekuwa nahodha wa Liverpool Jumapili hii alifunga mabao mawili na kufikisha mabao 16 katika EPL msimu huu, idadi ambayo ni kubwa kuliko yote yaliyofungwa na Spurs msimu huu.(P.T)
Mabao mengine ya Liverpool yalifungwa na Jordan Henderson, Jon Flanagan na Raheem Sterling.
Spurs walipata pigo zaidi baada ya Paulinho kutolewa nje kwa rafu mbaya ya kumrushia daluga Suarez kifuani, mchezo ambao kocha Villas-Boas alidai haikuwa haki kutolewa nje kwa madai kwamba hakufanya makusudi.
Liverpool kwa ushindi huo wamewashusha Chelsea kutoka nafasi ya pili, licha ya wote kuwa na pointi 33 nyumba ya Arsenal wanaoongoza kwa pointi 35.
Katika mechi nyingine, Manchester United walifanikiwa kupata ushindi ugenini walipocheza na Aston Villa jijini Birmingham, tena kwa mabao 3-0.
Mabao hayo yalifungwa na Danny Welbeck aliyepachika mawili na Tom Cleverly moja na kumpa ahueni kocha David Moyes aliyekuwa amechanganywa na vipigo mfululizo.
Kwingineko Norchich ya Chris Hughton ilikwenda sare ya 1-1 na Swansea katika mechi iliyopigwa Wales kwa Swansea.
Hadi mwisho wa raundi hii ya 16, timu nyingine iliyo kwenye nne bora ni Manchester City yenye pointi 32.
Nafasi ya tano inashikwa na Everton wneye pointi 31 na wanaofuatia na pointi zao kwenye mabano ni Newcastel na Spurs (27), Manchester United (25), Southampton (24) na Swansea (20).
Aston Villa na Hull wana pointi 19 katika nafasi ya 11 na 12, wakifuatiwa na Stoke na Norwich (18), Cardiff (17), West Bromwich Albion (15) na West Ham (14).
Tatu zilizo katika hali ngumu zaidi chini ya msimamo wa ligi ni Crystal Palace na Fulham zenye pointi 13 kila moja na Sunderland wanaoshika mkia kwa kuwa na pointi tisa.

pop up

 
Support : KARIBU TENA BONGO MASKANI
Copyright © 2011. BONGO MASKANI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA BONGO MASKANI
Proudly powered by Blogger