Kwanini Hotuba Ya JK Kumuaga Mandela Ilikuwa Bora?
NOTHING can come from NOTHING. Wamesema hili Wanafalsafa wa Uyunani ya Kale .
Nimemwona na kumsikiliza Rais wetu Jakaya Kikwete akizungumza kwenye siku muhimu ya kumuaga kwa mara ya mwisho Mzee wetu Nelson Mandela.
Muda wote wa hotuba yake, JK alibaki kwenye mstari kwa namna ile ile ya kuweka bayana kwa ulimwengu, kuwa ' msione vinaelea'.
Hakika alichofanya JK leo ndicho haswa alipaswa kukifanya, na amekifanya kwa kutumia weledi wake kwenye diplomasia na kuchanganya uzoefu wake kwenye uongozi wa kisiasa na dola kwa ujumla.
Ni kuitumia fursa ile ambapo macho na masikio ya dunia yalielekezwa Quni, kwa yeye rais kuiambia dunia, na si kuisubiri CNN au vyombo vya habari vya Kimagharibi kuifanya kazi hiyo, juu ya mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika ikiwamo mchango wa Tanzania kumfanya Mandela na viongozi wengine wa Kiafrika kuonekana kama walivyoonekana kwenye macho ya dunia.
Hakika, JK anastahili pongezi kwa kazi njema aliyoifanya leo ya kuiweka tena Tanzania katika ramani ya dunia, si tu kama nchi ile ya mbuga za wanyama na Mlima Kilimanjaro, bali ' Taifa Kubwa' lililochangia kushiriki mikakati ya ukombozi ikiwemo kutoa misaada ya silaha, mafunzo na hata makazi kwa wapigania ukombozi wa Afrika.(P.T)
Lakini, tujiulize pia kama Watanzania, katika aliyoyasema JK kule Quni, ni Watanzania wangapi wanayajua? Inahusu umuhimu wa kuipitia historia yetu ili, kama Watanzana, tuweze kumiliki ' K3'- Kujitambua, Kujiamini na kuthubutu. Imefika mahali tunaionea aibu hata historia yetu.
Na nyongeza katika yale aliyoyasema JK leo ni kumbukumbu ya kihistoria ambayo haitajwi pia, kuwa Baba wa Taifa , Mwalimu Nyerere, ndiye aliyempa hifadhi Tanzania, Rais wa Pili wa Afrika Kusini huru, Thabo Mbeki baada ya kutoroka Afrika Kusini. Baadae Thabo Mbeki akaenda kusoma Uingereza.
Jambo hilo linathibitishwa katika kitabu alichoandika msomi mahiri wa Afrika Kusini, William Gumede. Anasema;
" In 1962, Thabo slipped out of the country to which he would not return for twenty -eight years, travelling through Botswana to Rhodesia, where he was arrested and held in a Bulawayo prison for several weeks. The white Rhodesian authorities intended to deport him back to South Africa and waiting for security police, but British Labour MP, Barbara Castle intervened after being lobbied by the ANC, and Mbeki was granted asylum in Tanzania by President Julius Nyerere." ( William Gumede, Thabo Mbeki and The Search For Soul of The ANC, pg 36)
Naam, ni wakati sasa wa viongozi wengine, bila kujali itikadi zao, wanapokuwa kwenye majukwaa ya kimataifa, kuzitafuta fursa za kuonyesha yale ambayo huko nyuma tumekuwa na uwezo nayo, na bado, kama nchi, tunaweza kuaminika katika kutoa mchango wa uzoefu wetu kwenye masuala mbali mbali ya Kimataifa.