Wakati Serikali ikisema Daftari la Kudumu la Wapigakura litaboreshwa kwa ajili ya kura za maoni ya Katiba Mpya, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema haina mpango huo kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
Badala yake Nec imesema inajiandaa kuboresha daftari hilo kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili kuingiza wale wote waliotimiza miaka 18 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema jana kwamba itakuwa vigumu kuliboresha daftari hilo kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni utakaofanyika mwanzoni mwa mwaka 2014 kwa sababu muda uliobaki ni mfupi na hakuna fedha za kufanya hivyo.(E.L)
"Muda uliobaki kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni ni mfupi, itakuwa vigumu kwa tume kuliboresha daftari la wapigakura nchi nzima ila tunajiandaa kuliboresha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015," alisema Jaji Lubuva.
Alisema nchi ni kubwa kijiografia kiasi kwamba unahitajika muda mrefu kwa ajili ya kuliboresha daftari hilo na kwa vile zoezi la upigaji kura za maoni litafanyika mwanzoni mwa 2014, tume itakuwa imechelewa kufanya hivyo.
Kauli ya Serikali
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipoulizwa jana mjini Dodoma kuhusu tamko la Jaji Lubuva, alisema msimamo uliotolewa na Waziri Mkuu wiki iliyopita ndio msimamo wa Serikali.
"Serikali tunajiandaa, na wao (NEC) wanajua fedha za mwanzo tumeshapeleka na mchakato umeanza. Wameshakagua mashine zitakazotumika....process (mchakato) hii yote inalenga kura ya maoni," alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Lukuvi alisema inawezekana kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba Katiba Mpya itapatikana Aprili 26, mwaka huu ndiyo inayowachanganya, wanaona muda uliopo ni mfupi lakini hilo ni la Serikali na siyo tume.
Desemba 5, mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alivihakikishia vyama vya siasa na Watanzania kwamba Daftari la Kudumu la Wapigakura litaboreshwa kabla ya upigaji kura ya maoni juu ya Katiba Mpya. Hali kadhalika Pinda alisema Serikali itatumia daftari hilo la Nec katika upigaji kura ya maoni ya katiba kwa pande zote za Muungano.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati akihitimisha hotuba yake ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 ambapo suala la daftari la wapiga kura lilibua mvutano mkali. Wabunge wa Tanzania Bara walitaka daftari la wapiga kura liboreshwe kwanza, huku wale wa Zanzibar wakitaka wasio na vitambulisho vya ukaazi waruhusiwe kupiga kura kwa kutumia daftari la Nec
Pinda alisema daftari la kudumu la Nec kwa sasa lina orodha ya Watanzania wa Bara wanaoishi Zanzibar, lakini hawawezi kupiga kura kwenye uchaguzi ule wa ndani wa upande wa Zanzibar.
Uboreshaji Daftari
Mara ya mwisho daftari hilo kuboreshwa ilikuwa mwaka 2010 na sasa kuna idadi kubwa ya vijana waliofikisha umri wa miaka 18 ambao wanatakiwa kuwemo kwenye daftari hilo.
Sifa ya kupiga kura ya maoni ni mtu kuwa mwananchi kuandikishwa kwenye daftari hilo.
Uhuru wa Tume
Kuhusu uhuru wa tume hiyo, Jaji Lubuva alisema yeye na makamishna wa tume wako huru na hawaingiliwi na chombo chochote cha Serikali wala chama cha siasa katika kutekeleza majukumu yake.
"Haijawahi kutokea hata siku moja kwamba tume imeagizwa na kiongozi yeyote wa juu kuendesha uchaguzi kwa kupendelea chama au mgombea," alisema.
Alisema tume inafanya kazi zake kwa uhuru lakini kama wananchi wanataka mabadiliko yoyote kwenye Katiba Mpya kuhusu namna ya kupata tume, hilo ni suala la msingi. "Tume iko huru, ila wananchi wanaweza kuamua namna ya kupata Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo wanapenda iwe, sisi hatuna kipingamizi," alisema Jaji Lubuva.
Kauli za wanasiasa
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema kauli ya Nec inaashiria kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilidanganya Bunge na Watanzania wakati wa mjadala wa Muswada wa Kura ya Maoni kuwa daftari litaboreshwa kabla ya upigaji wa kura za maoni. Alisema kauli hiyo inaashiria kwamba wananchi waliopoteza kadi, waliokosa fursa wakati wa uboreshaji mwaka 2010 na waliofikisha umri wa kupiga kura watakoseshwa haki ya kupiga kura kuamua hatima ya nchi yao.
Mnyika alisema Nec imeamua kung'ang'ania daftari lenye kasoro ambalo limekuwa likilalamikiwa tangu mwaka 2010 kwamba linahitaji kuhakikiwa.
Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba alipotafutwa jana kuzungumzia hilo, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu, kama ilivyokuwa kwa James Mbatia wa NCCR-Mageuzi