TANZANIA Bara 'Kilimanjaro Stars', leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos, kumenyana na wenyeji, Kenya 'Harambee Stars' katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge kuanzia saa 7:00 mchana.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Stars chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen kufika Nusu Fainali ya michuano hiyo, baada ya mwaka jana pia mjini Kampala, Uganda ambako ilitolewa na wenyeji, Uganda 'The Cranes' kwa kufungwa mabao 3-0.(P.T)
Lakini Kim, amelipa kisasi kwa The Cranes, baada ya Stars kuivua ubingwa Uganda Jumamosi kwa kuitoa kwenye Robo Fainali, Uwanja wa County ya Mombasa, zamani Manispaa kwa penalti 3-2, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Baada ya kumaliza shughuli hiyo pevu, Kim anakabiliwa na jukumu lingine zito mbele yake, ambalo ni Nusu Fainali dhidi ya Kenya, ambayo imeonekana 'kubebwa' mno na marefa hadi sasa katika mashindano haya.
Kenya imekuwa ikipewa penalti katika mechi zote kuanzia hatua ya makundi hadi Robo Fainali na hali hiyo inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuendelea na leo pia Machakos.
Beki wa Azam FC, Joackins Atudo amepiga penalti nne na kufunga tatu hadi sasa, wakati moja alikosa katika mechi ya Kundi A dhidi ya Sudan Kusini.
Habari njema ni kwamba, kipa wa Stars, Ivo Mapunda anaheshimika mno kwa uhodari wa kucheza penalti, lakini pia Wakenya wanamuamini mno Atudo katika upigaji.
Mechi hiyo imeteka hisia za wengi na sababu za Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuipeleka Uwanja wa Kenyatta badala ya Nyayo, Nairobi ni kutokana na imani kwamba watu wa huko huishagilia mno Harambee Stars inapocheza.
Wakati Stars iliitoa Uganda, Kenya waliingia Nusu Fainali baada ya kuifunga 1-0 Rwanda 'Amavubi' kwa bao la penalti iliyotolewa katika mazingira ya utata iliyopigwa na Atudo kama kawaida.
Kenya ina ukuta imara, safu nzuri ya kiungo, lakini haina makali sana katika safu yake ya ushambuliaji, wakati Tanzania Bara japokuwa itamkosa kiungo wake, Salum Abubakar 'Sure Boy' aliyeonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Uganda, bado ina viungo wengine bora wa kuziba pengo hilo.
Kuna chipukizi Hassan Dilunga wa Ruvu Shooting na mkongwe Athumani Iddi 'Chuji' wa Yanga, ambao yeyote kati yao Kim anaweza kumpa jukumu la kuziba pengo la kiungo wa Azam FC, Sure Boy.
Stars ina ukuta imara kama ilivyo kwa safu ya kiungo na utamu zaidi ni safu yake ya ushambuliaji inayoundwa na wakali wawili wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu kwa pamoja na Mrisho Khalfan Ngassa wa Yanga.
Iwapo hali ya Ngassa haitakuwa imeimarika, hakuna shaka 'viberenge' vya Simba SC, Haroun Chanongo na Ramadhani Singano 'Messi' mmoja wao anaweza kuchukua nafasi na akafanya kazi nzuri- lakini pia kuna makinda mengine mawili ya Azam FC, Joseph Kimwaga na Farid Mussa pia wanaweza kucheza nafasi hiyo.
Litakuwa pengo kumkosa Ngassa kutokana na uzoefu wake ambao tayari anao hivi sasa kisoka, lakini pia itakuwa nafasi nzuri kwa chipukizi hao kuupambanua uwezo wao, iwapo watapewa nafasi.
Himid Mao amemaliza adhabu ya kadi na baada ya kuwa nje ya Uwanja katika mechi dhidi ya Uganda, leo anarudi kwenye mashindano na litakuwa jukumu la Kim kumchezesha kiraka huyo wa Azam, au kumpanga tena Michael Aidan wa Ruvu Shooting. Nusu Fainali nyingine ni kati ya Zambia na Sudan mjini Mombasa. Kila la heri Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars'.