Waona giza nene mbele yao, Uganda yaonya vita inanukia
DRC yazidisha mashaka kwa Uganda, Watanzania waonya
Hatua
ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kukataa kusaini
mkataba wa amani na kundi la waasi la M23, imepeleka kilio kwa kundi
hilo, na sasa wanalia njaa uhamishoni nchini Uganda.
Uganda, nchi ambayo ni msuluhishi wa mgogoro huo, imejikuta katika
wakati mgumu kwani kundi la waasi wa M23 wapatao 1,700 limekimbilia
nchini humo, ilhali Uganda ikiwa na jukumu la kusuluhisha waasi hao na
Serikali ya DRC.
Msemaji
wa Serikali ya DRC, Lambert Mende, mwishoni mwa wiki ametamka kuwa
Serikali yake ina wasiwasi kuwa Uganda ina maslahi binafsi na waasi wa
M23, hivyo hawako tayari kutia saini mkataba unaosimamiwa kwa mitego.
“Uganda sasa inaonekana kuwa sehemu ya mgogoro. Ina maslahi na M23,” alisema Mende.
Kauli
hii ya Mende imekuja siku chache baada ya DRC kukataa kutiliana saini
na waasi kwa maelezo kuwa M23 ni kundi lililotangaza kujivunja,
wamekimbilia Rwanda na Uganda, na hivyo kulipa sharti kubwa
wanalolikataa.
Sharti
hilo ni kuwa mkataba uwe na kipengele kinachowazuia M23 milele
kutoshika silaha na kuanzisha mapambano, hoja inayokataliwa na waasi,
huku Uganda ikizishawishi pande mbili zitie saini mkataba hivyo hivyo
ulivyo kwa maelezo kuwa yakitokea matatizo mbele ya safari utarekebishwa
tena.
Masharti
mengine wanayowapa waasi hao ni kuwa makamanda wapatao 100 waliokuwa
wanaongoza kundi la M23, wasiruhusiwe kuingia jeshini moja kwa moja, na
badala yake wapewe mafunzo ya kijeshi, huku wakiacha fursa ya kushitaki
wahalifu wa kivita watakaothibitika mbele ya safari kuwa walitenda
uhalifu dhidi ya binadamu.
Uganda,
ambayo sasa hivi ina mzigo mkubwa wa kulisha waasi hao waliowekwa
kambini nchini humo tangu Jumatatu (Novemba 4) kundi hilo lilipotangaza
kushindwa vita na kuweka silaha chini, inasema hali inayoiona ikiwa
waasi hao hawatahakikishiwa usalama wao, pato la fedha na kushirikishwa
serikalini, kuna wasiwasi kuwa wanaweza kurejea msituni.
“Hawa
ni binadamu. Njaa ikiwashika, usitarajie watasubiri kufa kwa njaa.
Wanaweza kurejea msituni,” alisema afisa mmoja wa Serikali ya Uganda.
Uganda
pia imetishia kwa mara nyingine mwishoni mwa wiki kuwa ikiwa suluhu
haitapatikana haraka, na DRC ikaendelea kuituhumu kuwa inashirikiana na
waasi wa M23, basi yenyewe itajitoa katika nafasi ya kuwa msuluhishi.
Kuhusiana
na tishio la Uganda kujitoa kwenye mazungumzo, Waziri Mdogo wa Mambo ya
Nje wa Uganda, Asumani Kiyingi, amesema: “Tumewasiliana na Umoja wa
Mataifa kupitia kwa Balozi wetu jijini New York, kwani tunataka kufahamu
iwapo kilichoandikwa kwenye vyombo vya habari ni cha kweli,” amesema.
“Ikiwa
Umoja wa Mataifa utathibitisha kuwa wataalamu wake wameandika taarifa
hizo za uongo [kuwa Uganda inaunga mkono M23], basi tutajitoa katika
jukumu la usuluhishi wa mgogoro wa DRC na waasi wa M23.”
M23
kwa upande wao walioanza vita Aprili 2012 wanamtuhumu Rais Joseph
Kabila kuwa wao ndiyo waliomsaidia baba yake, Laurent Kabila, kuingia
madarakani na hata makundi ya waasi yalipokuwa yanatishia kumuondoa
madarakani walimtetea, lakini alipoingia madarakani akawatekeleza.
Wataalamu
wanasema kuwa nchi za Uganda na Rwanda pamoja na kukaripiwa na jumuiya
ya kimataifa, zikaacha kukiunga mkono kikundi cha M23, hali iliyokifanya
kichapwe kama mtoto mdogo, sasa zimehamishia nguvu kwa makundi mengine
ya waasi yaliyopo kwenye misitu ya Congo.
Shutuma
kubwa zinazosukumwa kwa nchi hizi ni kuwa zimekuwa zikinunua madini na
mbao kutoka kwa waasi, hali inayoziingizia fedha nyingi za kigeni bila
kujali kuwa zinahatarisha maisha ya Wakongo wasio na hatima, taarifa
ambazo Serikali ya Uganda imeziita za ‘kipuuzi’.
Kikosi
Maalum cha Umoja wa Mataifa kinachoongozwa na Mtanzania, Brigedia
Jenerali James Mwakibolwa, kwa kuhusisha Brigedi Maalum ya SADC,
kimewachakaza M23 hadi wakasalimu amri, lakini wachambuzi wa mambo
wanasema kung’olewa kwa M23 si mwisho wa matatizo DRC.
Richard
Mugamba, Mhariri Mtendaji wa gazeti la the Citizen, ambaye amekuwa
akiripoti habari za waasi kwa kufika Goma, anasema M23 ni moja ya
makundi zaidi ya 17 yaliyoko mashariki mwa Congo.
“Kila
mtu anatambua kwamba M23 kuweka silaha chini ni furaha kwa Wakongo, ila
matatizo yao yana miaka 17. Tangu 1999 wamekufa watu milioni 5. M23
wamekuwapo kwa miezi 24, lakini mashariki mwa Congo kuna makundi kama
FDRL, Mai Mai, RCD-Goma, ADF, kuna vikundi 17 na vyote hivi viko
mashariki kwenye madini, kwenye mbao na mkaa.
“Ni
vyema kwamba M23 imeshindwa, lakini haiwezi kuwa suluhisho tangu 1996
walipommaliza Mabutu [Sese Seko Kukubanga wa Zabanga], wamekuwa
wakipigana. Kiongozi wa waasi Laurent Nkunda yuko Uganda (CNDD). Kuna
nchi ambazo zinatuhumiwa – Rwanda na Uganda zinatuhumiwa,” amesema
Mugamba. Hata kiongozi wa sasa wa M23, Kanali Sultani Makenga,
amekimbilia Uganda.
“Sisi
kama Tanzania tume-play role (tumetimiza wajibu) yetu. Kuna watu
wanataka haya makundi yawepo kwa sababu wanafanya biashara. Makenga
alikuwa ana-access dola 58 milioni mwaka jana, tuseme anapata dola
milioni 10, lazima wote wanafanya biashara.
“Watu
wote wanaohusika na Congo hebu wakae chini wazungumze. Mali zinauzwa
nje. Nikiwa Congo niliona vitu ambavyo nasema sawa kuna tatizo, lakini
mbona kuna mikono mingi tu. Kama hakuna amani Congo au kwa jirani yako,
wewe huwezi kuwa na amani. Angalia hali ya usalama kwa mikoa ya Kigoma
na Kagera.
“Jeshi
la UN lipo Congo kwa miaka 11, watu milioni 5 wameuawa. SADC
Intervention Brigade UN waliipinga awali, lakini angalia kazi iliyofanya
kwa miezi sita. Dunia kama ingekuwa na nia ya dhati hawa waasi wote
wangekuwa hawapo,” anasema Mugamba.
Mobhare
Matinyi, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, anasema M23 kama kikundi
kimekwisha kwa sababu makamanda wake wamejisalimisha, na kuna taarifa
kuwa Waziri wa Mashauri ya Nje wa Marekani, John Kerry, na Waziri Mkuu
wa Uingereza, David Cameron, walimpigia simu Rais wa Rwanda, Paul
Kagame, kumwambia asiingilie aache hiki kipigo kiishe.
“M23
imepigika, haina uwezo wa kuibuka tena, lakini bado kuna hatari. Kwa
kuwa Uganda viongozi wake wana maslahi binafsi nchini Congo na Rwanda
ina maslahi ya kitaifa Congo, kuna uwezekano wakaanzisha insurgence
groups (makundi ya waasi) kuleta shida kwa Congo waendelee kuvuna,”
Matinyi ameiambia JAMHURI.
Anasema
bado kuna makundi yanayopigana yenyewe kwa wenyewe, baadhi ya makundi
hayo ni kama FDLR, Democratic Forces for Liberation of Rwanda, mabaki ya
Interahamwe na Banyamulenge ambao bado ni tishio.
“Majeshi
yetu Tanzania kihistoria ni nchi yenye msingi wa utu, usawa na haki.
Ndiyo maana Tanzania imekuwa ikitoa majeshi yake kumtetea Mwafrika na
kumtetea binadamu. Tulipoitikia kwenda Congo ilikuwa ni kumtetea
Mwafrika, hatuwezi kukaa miaka 20, 30 watu wakiuawa sisi tunaangalia
tu,” anasema.
Swali
ni je, njaa ikiendelea kuwasumbua waasi wa M23 hawatarudi msituni?
Wachambuzi wanasema mkataba wa amani unapaswa kuharakishwa.