Mgogoro
ndani ya Chadema umezidi kupamba moto baada ya Kamati Kuu kuwavua
uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa,
Said Arfi akiandika barua ya kujiuzulu.
Zitto
alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati
Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa kukisaliti chama.(HD)
Taarifa
zilisema hoja ya kukisaliti chama pia ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha
Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi
mkuu uliopita na ndiyo sababu ya kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali ya
kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14
wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki
na wadhifa wa ubunge wake wa Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye
Kamati ya Bunge.
Zitto azungumza
Mara
baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Zitto aliliambia gazeti hili, "Sina
cha kueleza, kikao kilikwenda vizuri na taarifa rasmi ya chama kuhusu
uamuzi wa kikao itatolewa baadaye mchana (jana saa nane mchana),
tusubiri Kamanda."
Arfi ajiuzulu
Makamu
Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda
Mjini, jana aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya uongozi wa chama,
akisema; "...kuchoshwa na unafiki unaoendelea ndani ya chama. Napenda
ifahamike pia kwangu masilahi ya wapigakura, wakazi na wananchi wa
Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo
basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.
Katika
barua hiyo anasema amechochwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa
kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa
katika uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
"Kwa
kipindi kirefu zimekuwepo shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka uhusiano
wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu. Pamoja na kulijadili katika vikao
kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka kwa nini alipita bila
kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo,
lakini hamsemi kwa nini. Majimbo mengine 16 nchini yalipita bila
kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe? Huu ni unafiki wa kupindukia.
Vilevile,
katika barua hiyo, Arfi anasema amechukizwa na kauli ya mwasisi wa
chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
"Aidha
mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei
kutuchagulia viongozi. Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu
na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi
wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa
mali binafsi.Kwa kusema ukweli na kusimamia ukweli daima itabakia kuwa
lengo langu katika maisha yangu siku zote hata kama itanigharimu maisha
yangu."
Hata
hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa alipoulizwa kwa njia ya
simu kuhusu barua ya Arfi ya kujiuzulu uongozi, alisema; "Mimi
nimekwishaondoka ofisini."
Taarifa ya chama
Akitangaza
uamuzi wa Kamati Kuu jana Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema,
Zitto, Dk Mkumbo na Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba
walikuwa na mtandao wa kukiua chama hicho, huku wakitengeneza tuhuma za
kuwachafua Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk
Willbroad Slaa.
Alisema
kuwa kamati kuu ilibaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza
malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa 'Mkakati wa
Mabadiliko 2013', ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita 'Mtandao wa
Ushindi'.
"Kikundi
hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM),
Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne hatujamtambua kwa sasa
yeye anatumia jina la M2" alisema Lissu.
Alisema
wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu Dk Mkumbo alikiri kuwa mhusika mkuu wa
mtandao huo ni Zitto, lakini Zitto alikana kuutambua waraka huo licha ya
kueleza unamhusu kwa kuwa umetaja jina lake, kauli ambayo alidai Kamati
Kuu haikutaka kuiamini.
Huku
akieleza jinsi watu hao walivyokuwa wakiwasiliana na kupanga mikakati ya
kuimaliza Chadema kwa siri chini ya ufadhili wa fedha kutoka kwa Zitto,
Lissu alisema Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani alikuwa akitumiwa na
Chama Tawala (CCM) kuimaliza Chadema.
"Mkakati
wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichanachana katiba ya
chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya chama chetu na utaratibu wetu
wa kikatiba. Hatuwezi kunyamazia mkakati huu wa kutumaliza, uvumilivu
umefika kikomo," alisema.
Uamuzi
Alisema
kutokana na hali hiyo kamati kuu iliamuru wahusika wote wavuliwe
nyadhifa zao zote za uongozi wa chama, kukubaliana kuunda timu ndogo ya
pamoja ya watendaji wa sekretarieti ya makao makuu ya chama hicho ili
kumtambua mtu wa nne (M2).
"Kamati
ya Bunge imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa
nafasi zote za Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia
wote wanatakiwa kujieleza ndani ya siku 14 kwa nini wasivuliwe uanachama
na watapewa fursa ya kujitetea," alisema.Alisema Kamati Kuu itakutana
kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatima ya watuhumiwa hao.
Kauli ya Mbowe
Awali
Mbowe alipinga madai kuwa Zitto ameondolewa kwa kuwa alikuwa akitaka
kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, akasisitiza kuwa uamuzi huo
umefanyika kwa kuwa Chadema ni chama cha watu, siyo mali ya mtu
binafsi.
Mvutano Zitto, Lema
Kwa zaidi ya wiki mbili Zitto amekuwa akilumbana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Alimtuhumu
mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni,
lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii
nchini.
Lema
aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala
hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari
na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Zitto
alijibu kuwa tangu siku nyingi alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi au
mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema
tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma (POAC), alipiga marufuku posho na pia aliwahi kuwashtaki kwa
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua
posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia
alipata msukosuko mwingine baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa
'Taarifa ya Siri ya Chadema' iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na
CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa kuihujumu Chadema.
Pia,
Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama
vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu
za Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo
isimamishwe.Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa
inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo. Vyama vinavyopata ruzuku ya
Serikali ni vile vyenye wabunge Chadema, CCM, UDP, TLP, CUF na
NCCR-Mageuzi.
Mvutano kikaoni
Wakati
wajumbe wa kikao hicho wakivutana, Zitto alikuwa njiani akirejea kutoka
Sudan Kusini, ambapo alienda na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC).
Taarifa
kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, baada ya kuibuka sintofahamu
hiyo, Mbowe aliwapoza wajumbe wa kikao hicho, akiwaeleza kuwa haitakuwa
busara kumjadili mtu ambaye hayupo.
"Mbowe
alipendekeza kuwa ajenda hiyo iwekwe kando na itajadiliwa baadaye
kutokana na Zitto kutokuwepo katika kikao hicho," zilieleza habari hizo.
Baadaye
Zitto alituma ujumbe ambao ulitangazwa kwa wajumbe wote, kwamba alikuwa
njiani kurejea Tanzania, kwamba akifika moja kwa moja atakwenda katika
kikao hicho.
Zitto awasili, mzozo waibuka
Kama vile
alikuwa akisubiriwa yeye, mara baada ya kufika katika ukumbi huo saa
2:23 usiku huku akisindikizwa na walinzi wanne, mvutano mkali uliibuka
katika ukumbi huo na mara kadhaa walinzi wa chama hicho, Red Brigade
walionekana kukaa tayari mlangoni kuzuia vurugu kama ingetokea.
Gazeti
hili lilikuwa nje ya ukumbi huo na mara kadhaa lilisikia sauti za
malumbano za baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Zitto, Mbowe na
Lema.
Wakati
wakitoa maelezo kwa nyakati tofauti Lema na Zitto walishutumiana huku
kila mmoja akimtaja mwenzake kuwa anatumia vibaya nafasi yake na
mitandao ya kijamii.
"Tatizo
lake ni kutumia mitandao ya kijamii kueleza mambo ya chama wakati akijua
siyo utaratibu, ugomvi wangu naye kwa kiasi kikubwa uko hapo,"
alisikika akisema Lema.
Kuna
wakati yaliibuka malumbano makali huku sauti za juu zikisikika kutoka
ndani ya ukumbi huo, kati ya Zitto, Lema na Mbowe.Taarifa kutoka ndani
ya kikao hicho zinaeleza kuwa Dk Mkumbo alikumbwa na rungu hilo baada ya
kubainika kuwa alikuwa ameanda taarifa za siri ambazo zilikutwa katika
kompyuta mpakato (laptop) ya Mwigamba ambayo alinyang'anywa baada ya
kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Kikao
hicho kilimalizika saa 10:00 alfajiri huku maamuzi hayo yakifanywa siri
na Mbowe alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa za Zitto na Dk Mkumbo
kuvuliwa uongozi," alisema , "Taarifa zitatolewa baadaye mchana."
Wasomi wazungumza
Akizungumza
na gazeti hili jana, Profesa Gaudence Mpangala alisema Chadema ni chama
kikubwa kinachoweza kushinda uchaguzi mkuu ujao hivyo kinapaswa kuwa na
viongozi walioshikamana na kuwa na nia moja.
Aliongeza
kuwa endapo wapo viongozi wanaoonekana kwenda kinyume na viongozi
wenzao na kwenda kinyume na misimamo ya Chama, kinayo haki ya kufanya
maamuzi ya namna yoyote yenye lengo la kukinusuru.
"Chadema
ni chama kikubwa kinachoweza kushika dola...kinahitaji mshikamano mkubwa
kwa viongozi wake na kuhakikisha hawatokei wasaliti....kama ni kweli
waliosimamishwa ni wasaliti ni halali kabisa" anasema Profesa Mpangala.
Naye
aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT, Dk Charles Kitima alisema
wakati umefika kwa vyama vya siasa kutambua kuwa uwepo wa demokrasia
ndani ya vyama vingi vya siasa nchini ni kusahihishana na kujisahihisha.
Dk Kitima
alisema kuwa na mitazamo tofauti siyo usaliti ni demokrasia na kusema
endapo mtu au kiongozi anafanya kitendo cha kuvunja katiba ya nchi huyo
moja kwa moja anakuwa mkosaji.
Mbunge wa
Jimbo la Wawi (CUF), Hamad Rashid anasema matukio ya kufukuzana na
kutuhumiana baina ya viongozi yanayofanywa na watendaji mkuu wa vyama
vya upinzani yatasababisha upinzani uzidi kudidimia na kudumaa.
Alisema
vyama vya siasa vimekuwa na usultani wa kuonekana kuwa vinapaswa
kuongozwa na baadhi ya watu, na wengine wenye uwezo na mawazo mapya na
yasiyopendwa na wakubwa anatafutiwa mbinu ya kuondoka.
Rashid
alisema hali hiyo inasababishwa na kukosekana kwa mfumo mzuri wa uongozi
ndani ya vyama vya siasa, ambapo anasema vyama haviongozwi kama taasisi
na badala yake vinaongozwa kama mali za watu.
"Hili
linalotokea Chadema sasa ni matokeo ya mfumo mbovu wa uongozi ndani ya
vyama vya siasa nchini....vingi haviongozwi kama taasisi."
alisema.CHANZO MWANANCHI