GOR MAHIA YAMKOMALIA KIPA IVO MAPUNDA-YASEMA HAENDI POPOTE BADO WANAMUHITAJI
KLABU ya Gor Mahia ya Kenya haina presha na kipa wake Ivo Mapunda na imesisitiza kumuongezea mkataba baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji.
Mapunda, ambaye mkataba wake unamalizika mwezi huu, ndiye kipa namba moja wa Kilimanjaro Stars ambayo inacheza robo fainali dhidi ya Uganda leo Jumamosi mjini Mombasa.
Makamu Mwenyekiti wa Gor Mahia, David Kilo alisema watamuongezea mchezaji huyo mkataba na mpaka sasa wanajua ni mchezaji wao.
“Hakuna kilichobadilika mpaka sasa Ivo ni mchezaji wetu na tunasubiri tu imalizike michuano ya Chalenji tukae naye mezani tuingie makubaliano mapya,” alisema David.
Kiongozi huyo alikiri kwamba wamesikia kwamba kipa huyo amekuwa akiwindwa na timu nyingine lakini wao wanaamini atasaini nao mkataba mpya.
Simba imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumsajili kipa huyo ingawa ujio wa Yaw Berko unaweza ukawashawishi kuachana naye. Ivo ameonyesha kiwango kikubwa kwenye michuano ya Chalenji inayoendelea na kuwa kikwazo kwa washambuliaji wakorofi wa timu pinzani.
Kabla ya kutua Gor Mahia, Mapunda amewahi kuzidakia klabu za Prisons na Yanga. Aliyewahi kuwa kocha wa Stars, Marcio Maximo pia alipenda kumpa nafasi Ivo dhidi ya makipa wengine.