.
Ng'ombe
dume (fahali) atachinjwa kisha kuwekwa katika kaburi atakamozikwa Rais
wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela, Kijiji cha
Qunu, Mthatha Jimbo la Eastern Cape Jumapili hii.
Viongozi
wa kimila wa Kabila la AbaThembu wametoa mwito kwa Serikali ya Afrika
Kusini isiingilie taratibu za mazishi ya kiongozi huyo na kuonya kwamba
ikifanya hivyo, 'Mandela hatapokewa na miungu' na kwamba roho yake
inaweza kurejea na kuathiri familia.(HD)
"Jumapili
baada ya mwili wake kuwekwa katika kaburi lake, taratibu zote za kimila
zitafanywa na Himaya ya Kifalme," alisema Kiongozi wa Jamii ya Xhosa,
Nokuzola Mndende baada ya kutembelea familia ya Mandela, nyumbani kwao
Houghton, Johannesburg na kuongeza:
"Zitakuwa
ni mila na desturi za jadi, Serikali inapaswa kutupa nafasi na
isituingilie. Fahali (ng'ombe dume) atachinjwa kwa ajili ya
kumsindikiza, ni familia ya Mandela pekee watakaohusika na taratibu hizi
za kumwandalia safari njema."
Mandela
anazaliwa katika Kabila la AbaThembu ambalo linazungumza Ki- Xhosa na
kwa mujibu wa taratibu za kabila hilo, hata mwili wake utashushwa
kaburini na viongozi wa kimila.
Hata
hivyo, habari zaidi kutoka Qunu zinasema licha ya taratibu za kimila,
pia kutakuwapo taratibu za Dini ya Kikristo, ambayo Mandela alikuwa
muumini wake.
Kusafirishwa Jumamosi
Jumamosi
Decemba 14, mwili wa Mandela utasafrishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa
Jeshi wa Waterkloof, Pretoria hadi Mthatha, Eastern Cape kwa ajili ya
mazishi Jumapili.
Viongozi wa juu wa Chama Tawala cha ANC, watatoa heshima za mwisho muda mfupi kabla ya mwili huo kusafirishwa.
Taarifa
ya Idara ya Habari na Mawasiliano ya Afrika Kusini (GICS), ilisema Jeshi
la Afrika Kusini (SANDF), ndilo litakaloongoza shughuli zote za kuagwa
kwa mwili wa Mandela.
Gwaride
la heshima la askari wa SANDF litausindikiza mwili wa Mandela uwanjani
hapo na baadaye gwaride kama hilo litatoa heshima, wakati mwili huo
utakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha, huku askari wake
wakihusika na kuuchukua kutoka kwenye ndege.
Jeneza
lililobeba mwili wa Mandela litawekwa katika gari jingine maalumu. Wimbo
wa Taifa utapigwa ukiongozwa na SANDF, wakati heshima za kijeshi
zikitolewa.Taarifa hiyo ya Serikali inasema baada ya taratibu hizo,
mwili huo wa Mandela utasafirishwa hadi Kijijini Qunu ambako Kabila la
AbaThembu watafanya taratibu za kimila.
Hitimisho
la siku 10 za maombolezo ya msiba wa Mandela itakuwa Jumapili, Desemba
15 wakati kiongozi huyo atakapozikwa katika makaburi ya familia.
Wakati wa
mazishi SANDF pia wamepewa jukumu la kusimamia upelekaji jeneza
makaburini na heshima za kitaifa zitatolea pamoja na wimbo wa Taifa
kupigwa kabla ya maziko.:CHANZO MWANANCHI.