JESHI
la Polisi Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya limemtia mbaroni
askari wa Kikosi cha KMKM, Hussein Soud Hussein (30) baada ya kukamatwa
na dawa za kulevya jumla ya kete 270 katika eneo la Darajabovu mjini
Zanzibar.
Naibu
Mkurugenzi wa Makosa ya Upelelezi na Makosa ya Jinai Yussuf Ilembo
alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo na kusema inasikitisha sana
kuona askari ambaye ndio tegemeo la kupambana na vita dhidi ya dawa za
kulevya anajishughulisha na biashara hiyo haramu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa |
“Ni
kweli tumemkamata kijana mmoja Hussein Soud Hussein ambaye baada ya
kumfanyia usaili alikiri na kuthibitisha kwamba yeye ni askari wa Kikosi
cha KMKM na tuliona kitambulisho chake,” alisema Ilembo.
Ilembo
alisema askari huyo alikamatwa ikiwa sehemu ya msako unaoendelea wa
Jeshi la Polisi pamoja na Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya
kuwatafuta wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo.
Kukamatwa
kwa askari huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambao
walichukizwa na tabia yake ya kufanya biashara ya dawa za kulevya wakati
akiwa askari wa ulinzi.
Alisema
kwa sasa Polisi wapo katika doria endelevu ya kuwatafuta vijana
wanaofanya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo ya mjini na
vijijini.
Taarifa
zaidi ziliopo sasa kwa mujibu wa Jeshi la Polisi ni kwamba biashara ya
dawa za kulevya hufanywa zaidi vijijini kutokana na msako wa Polisi
Jamii ulioshamiri mjini ambao hautoi nafasi kwa wafanyabiashara hao
kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Chanzo: Habari Leo