Dk Slaa yuko mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya
ziara yake ya siku 11 kutembelea Mikoa ya Shinyanga na Kigoma kukagua na
kuimarisha uhai wa chama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Uwanja wa Mwenge Kakonko, Dk Slaa alisema Chadema ni chama imara
na kinaendeshwa kwa misingi ya katiba na kanuni.
“Hakuna kiongozi aliye juu ya katiba, ninawaasa wote wanaobeba mabango kujiangalia kwa kuwa ninafahamu wanatumiwa.”
Kabla ya kupokewa kwa mabango hayo, Dk Slaa
aliyewasili Kakonko saa 5:11 asubuhi akitokea Wilaya ya Kahama,
Shinyanga alikwenda moja kwa moja katika Kata ya Mhange ambako alifanya
mkutano wa hadhara.
Dk Slaa alikumbana na mabango hayo saa 8:45 mchana msafara wake ulipowasili Kakonko Mjini ukitokea Mhange.
Wakati Dk Slaa akiingia katika uwanja wa mkutano,
ulio jirani na Ofisi za CCM Wilaya ya Kakonko, kuliibuka kundi la vijana
wapatao watano wakiwa na mabango mkononi na kuanza kukimbia kuyafuata
magari matatu ya msafara wa Dk Slaa huku wakionyesha mabango yao. Hatua
hiyo iliwafanya polisi waliokuwapo eneo hilo la mkutano kuwazuia na
kuanza kuwatimua lakini mara baada ya Dk Slaa kuteremka katika gari yake
na kuingia uwanjani hapo, aliomba kipaza sauti na kuwataka askari hao
kuacha kuwatimua wenye mabango. “Naomba msiwaondoe waacheni waje...
waruhusuni kwenye mkutano na mabango yao. Waacheni waje hapa …
msiwazuie, waacheni waonyeshe mabango yao na muwaruhusu tu wapite hapa
mbele, msiwapige tafadhali,” alisema Dk Slaa.
Baada ya kauli hiyo, polisi waliwaruhusu vijana
hao watano ambao walibakiwa na mabango manne, moja likiwa limechanika
walipokuwa wanawazuia.
Mabango hayo yaliyokuwa na maandishi ya aina moja,
yalikuwa na ujumbe uliosomeka: “Tanzania Kigoma Kakonko bila Zitto
Haiwezekani”, ‘Mhe. Slaa, Mhe. Mbowe mnatakiwa kujiuzuru mara moja” na
jingine lilisomeka; “Hatupo tayari kwa kusikiliza lolote bila ya Zitto”.
Mara baada ya kupanda jukwaani Dk Slaa aliwataka
tena wenye mabango kusogea karibu na jukwaa kuu alipokuwa amesimama na
kuanza kuwauliza maswali vijana hao iwapo wanajua Katiba ya Chadema na
kama wana kadi za chama. “Naomba niwaulize, hivi nyie wenye mabango
mnaijua Katiba ya Chadema?” Walimjibu: “Hapana.” Dk Slaa akawauliza
tena: “Sasa mnadai nini kwa mabango yenu kama hamjui Katiba ya Chadema?”
Mmoja wa walioshika mabango hayo alijibu: “Mtetezi wetu Zitto.”
Kutokana na hali hiyo Dk Slaa aliwauliza, atakuwa
amekosea akiwakabidhi kwa Polisi kuwa siyo wanachama wa Chadema lakini
wanafanya vurugu katika mkutano halali?